BOIPLUS SPORTS BLOG
MSHAMBULIAJI Mbwana Samatta amechukuwa tuzo ya Mfungaji Bora wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika huku timu yake ya TP Mazembe ikitwaa ubingwa baada ya kuifunga USM Alger ya Algeria, mechi hiyo imechezwa Uwanja wa TP Mazembe jijini Lubumbashi.

Mazembe imetwaa ubingwa huo baada ya kuwafunga waarabu hao kwa jumla ya mabao 4-1 ambapo mechi ya kwanza iliyocheza Algeria, Mazembe walishinda bao 2-0 na mechi ya fainali pia ikimalizika kwa bao 2-0.

Samatta ametwaa tuzo hiyo baada ya kufikisha mabao saba ambapo kwenye mechi hiyo amefunga bao la penalti dakika ya 75 baada ya wachezaji wa USMA kumchezea rafu mchezaji wa Mazembe huku bao la pili likifungwa na Rogers Assale dakika ya 90 akipigiwa pande na Samatta .Katika kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa kujihami huku zikishambuliana kwa vipindi na mpaka wanakwenda mapumziko hakuna aliyefanikiwa kutikisa nyavu za mpinzani wake.

Katika kipindi hicho Mazembe walifanikiwa kupata kona ambazo zote hazikuzaa matunda baada ya kuokolewa na wapinzani wao ingawa kipindi cha pili Mazembe walipata nafasi nyingi lakini hawakuweza kuzitumia vizuri.Kwa ubingwa huo, Mazembe wamejinyakulia kitita cha dola 1.5 milioni wakati USMA wao wakiondoka na dola 1 milioni. Samatta na Thomas Ulimwengu ni wachezaji wa kwanza kutoka Tanzania kufanikiwa kutwaa Kombe la Mabingwa wa Afrika kwa kuisaidia Mazembe ambayo hii ni mara yao ya tano kutwaa ubingwa huo.

Kwa upande wa Samatta ndiye Mtanzania wa kwanza kunyakua kiatu cha Dhahabu kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika hivyo amejiwekea rekodi nzuri katika soko la kimataifa ambapo amefanikiwa kuingia kwenye kinyang'anyiro cha wachezaji 10 wanaowania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika anayecheza klabu za Afrika zitakazofanyika Januari, Nigeria.

Post a Comment

 
Top