BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
STRAIKA wa Gor Mahia ya Kenya, Michael Olunga amefurahi timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya (KPL) huku akisema ametimiza malengo aliyojiwekea ingawa si mfungaji bora wa ligi hiyo.

Akizungumza na BOIPLUS, Olunga ambaye alikuwa akitajwa kuwaniwa na Simba pamoja na Yanga wakati wa michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika jijini Dar es Salaam alisema kuwa alipojiunga na timu hiyo msimu huu alijiwekea malengo makuu mawili ambayo ni kuisadia timu kutetea ubingwa wake pamoja na kufunga  idadi ya mabao 16 kwa msimu mzima.


Olunga alisema kuwa amefurahi kuona malengo hayo yametimia na kuvuka malengo ya mabao aliyojiweka ambapo amemaliza ligi akiwa amefunga mabao 19 wakati Mfungaji Bora, Jesse Were yeye amemaliza na mabao 22.

"Nashukuru malengo yangu yametimia na mengine yamepitiliza, nilipanga nifikishe mabao 16 lakini nimefikisha mabao 19 hilo ni jambo kubwa sana kwangu, pia timu yangu imetwaa ubingwa wa ligi," alisema Olunga.

Huu ni ubingwa wa kwanza kwa Olunga tangu ajiunge na timu hiyo aliyosajiliwa kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Thika United ambayo pia ni ya ligi kuu.

Post a Comment

 
Top