BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Boniface Mkwassa amesema kuwa bado wana nafasi ya kuwatoa Algeria ugenini kama wapinzani wao hawatatumia mbinu chafu za nje ya uwanja.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa jana Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Stars ilitoka sare ya bao 2-2 ambapo mechi ya marudiano itachezwa keshokutwa Jumanne nchini Algeria.


Mkwassa alisema kuwa Algeria ni timu ya kawaida na tayari wamewasoma wapinzani wao ambao alisema wamekuwa wepesi kufungika huku akikiri mabadiliko aliyoyafanya ya kuwatoa Elius Maguli na Mudathir Yahaya na kuwaingiza Mrisho Ngassa na Said Ndemla ndiyo yaliyowaangusha katika mechi ya jana.

''Mechi ilikuwa yetu kabisa kwani wachezaji wamecheza kwa kupambana na kufanikiwa kushinda mabao mawili ingawa wapinzani wetu walisawazisha yote. Algeria ni timu ya kawaida na inafungika kirahisi kama hakutakuwa na mbinu chafu mechi ya marudiano basi tutawatoa kwao,'' alisema Mkwassa.

Mkwassa alisema alimtumia Maguli kwani ni mchezaji anayeweza kufunga, mpambanaji na ana nguvu lakini alimwingiza Ngassa ili kuongeza mashambulizi. Maguli alifunga bao moja huku Mbwana Samatta naye akifunga moja.
Stars imeondoka leo kuelekea Algeria ambako watalazimika kuifunga bao 1-0 au sare ya bao 3-3 ili waweze kusonga mbele. Algeria wao waliondoka jana usiku bada ya mechi hiyo kwani walikuja na Ndege ya kukodi.

Post a Comment

 
Top