BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Mbeya
KOCHA Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema  kuwa uchezaji wa straika wa TP Mazembe ya DR Congo, Mbwana Samatta  akiwa klabuni kwake ni tofauti kabisa na anavyocheza akiwa na timu ya Taifa 'Taifa Stars'.

Akizungumza na BOIPLUS katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe jijini Mbeya akiwa anarejea jijini Dar es Salaam kutoka mapumziko ya siku mbili, Mwambusi alisema ametazama mechi ya fainali ya CAF iliyopigwa Jumapili iliyopita jijini Lubumbashi kati ya Mazembe na USM Alger ya Algeria na Mazembe kuibuka mabingwa kwa jumla ya mabao 4-1 na kuona jinsi wachezaji wa kiungo wa Mazembe wanavyomlisha mipira Samatta ni tofauti kabisa na wanavyofanya viungo wa Stars.

Mbwana Samatta


"Samatta si mpiganaji kama alivyo mwenzake Thomas Ulimwengu, ila ni mzuri sana kwenye kumalizia, kule Mazembe naona wanamtumia vizuri kwa kumlisha mipira mizuri ya mwisho na ndio sababu anawafungia mabao mengi hadi kuibuka mfungaji bora wa michuano mikubwa kama Klabu Bingwa Afrika,'' alisema mtaalamu huyo wa utimamu wa viungo mwili.

Mwambusi ambaye aligoma kabisa kuizungumzia Yanga kwa madai kuwa kocha mkuu, Hans Pluijm ndiye msemaji wa masuala yote ya kiufundi ya timu aliongeza kwa kusema kuwa uwezo wa Samatta hauendani kabisa na matunda anayoipatia Stars huku akisisitiza ni lazima kuwe na mabadiliko.

"Ni lazima Samatta abadilike akiwa Stars kwa kucheza kwa kupambana zaidi ya afanyavyo sasa au vinginevyo basi viungo wa Stars wajifunze kutoka kwa viungo wa Mazembe jinsi ya kumchezesha mtaalamu huyo wa mabao,'' alifafanua kitaalamu.

Mwambusi kushoto akiwa na mwandishi wa BOIPLUS Songwe Airport, Mbeya


Akielezea mechi ya Stars na Algeria itakayopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi Mwambusi alisema ni mechi ngumu na wachezaji wa Stars wanapaswa kuongeza kujituma zaidi.

"Mechi ngumu sana hii mdogo wangu, Algeria wapo katika kiwango cha juu sana na ili Stars ipate ushindi ni lazima wachezaji wetu wajitoe kwa zaidi ya hata uwezo wao. Hata hivyo hawana sababu za kushindwa kujitoa kwa moyo wote, wanapata mahitaji yote muhimu na kwa kiwango stahiki tofauti na hapo zamani,'' alisema  Mwambusi.

Post a Comment

 
Top