BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
STRAIKA wa Simba, Msenegal Pape N'Daw amesema kuwa hana tatizo la kuondoka Simba kwani walikwishamalizana na klabu hiyo na sasa anafanya mazoezi na Wekundu hao wa Msimbazi akisubiri kukamilisha mambo yake ya safari.

Wakati wenzake wakipewa mapumziko ya muda mfupi, Pape hakuweza kuondoka nchini akisubiri kibali chake cha kazi kwani anakwenda Afrika Kusini kucheza katika moja ya timu ya nchini humo.


Tangu Simba waanze mazoezi, Jumatatu Pape amekuwa akifanya nao mazoezi na kusisitiza kuwa mambo yake yakikamilika ataondoka nchini "Tulimalizana na viongozi wa Simba muda mrefu, nafikiri kuna mambo sijaweza kuyatimiza ndiyo maana siwezi kuendelea kuichezea timu hii, nitaondoka na wala sina tatizo lolote na klabu, kuna mambo nilikuwa nakamilisha pia nimejifunza mengi tangu niwe na timu hii,".

Rais wa Simba, Evans Aveva naye amefafanua "Hatuna mawazo ya kumwongeza mkataba Pape, ikiwa na maana ligi itakapoanza hatutakuwa naye, kuna baadhi ya vitu alikuwa anaweka sawa tu ndiyo maana yupo mpaka sasa na ninafikiri vimekamilika,".

Simba pia ilimtema Simon Sserunkuma ambaye tayari alipewa barua ya kujulishwa kuwa hawataweza kuendelea naye na sasa yupo nchini kwao Uganda. Upande wa Pape yeye alikuwa akiichezea Simba kwa mkopo wa miezi mitatu ambayo tayari imemalizika.

Post a Comment

 
Top