BOIPLUS SPORTS BLOG

UKISTAAJABU ya Mussa utaona ya Firauni. Licha ya timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars' kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Cape Verde kwenye mchezo wa awali wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018, bado hadi muda huu hawajaondoka Nairobi kuifuata timu hiyo kwa ajili ya mchezo wa marudiano uliopangwa kupigwa kesho jijini Praia.


Kwa mujibu wa mtandao wa FUTAA.COM wa Kenya, safari hiyo iliyopaswa kuanza saa nne asubuhi kwa ndege ya kukodi ya kampuni ya Fly 540 kwenye Uwanja wa Ndege wa Wilson ilikuwa haijaanza hadi majira ya saa 12 jioni hii kwa madai kuwa wamiliki wa ndege wametaka kulipwa pesa yote kabla ya kuanza safari.

Kitendo cha wachezaji kuambiwa warejeshe pasi zao za kuingilia kwenye ndege 'boarding pass' ni ishara kwamba kuna kila dalili kuwa safari hii itaahirishwa kwa siku ya leo ambapo ni masaa machache tu kabla ya muda wa mechi hiyo ya marudiano. Safari ya kutoka Nairobi hadi Praia ni ya masaa yasiyopungua manane kwa ndege.


Akizungumza na mtandao huo, msemaji wa Shirikisho la Soka nchini Kenya (FKF), John Kariuki, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwavile yupo nje ya Nairobi.

"Sijui chochote kuhusu kinachoendea huko Uwanja wa Ndege kwavile nipo nje ya Nairobi, siwezi kusema kama safari imeahirishwa au vipi,''alisema Kariuki.

Endelea kutembelea BOIPLUS ili kujua hatma ya safari ya Harambee Stars.

Post a Comment

 
Top