BOIPLUS SPORTS BLOGMbwana Samatta (kulia) na Thomas Ulimwengu (kushoto)
FAMILIA ya straika wa TP Mazembe, Mbwana Samatta imepanga kumfanyia 'suprise' mchezaji huyo mara tu atakapowasili nchini na kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars' ambacho kimepiga kambi nchini Afrika Kusini huku baba yake mzazi Ally Pazi Samatta akitokwa na machozi ya furaha kwa hatua aliyofikia mwanaye.

Jana straika huyo alitwaa tuzo ya Mfungaji Bora katika michuano ya Mabingwa wa Afrika akiwa amefikisha mabao nane huku timu yake ya TP Mazembe ikitwaa ubingwa huo ikiwa ni mara yao ya tano.

Mzee Samatta alisema kuwa familia nzima imefurahishwa na hatua aliyofikia ndugu yao kwani ni jambo ambalo halijawahi kutokea  katika soka la Tanzania na kwamba Samatta ameitangaza vyema familia yao pamoja na nchi ya Tanzania kwenye hatua ya kimataifa.

"Tumepanga kumfanyia kitu ambacho hatujawahi kumfanyia tangu aanze kucheza soka, kwamaana kwamba katika maisha yake yote ya soka, kiukweli niliposikia ametangazwa Mfungaji Bora, niliamua kuwapigia wanangu wote waliopo mikoani ili waje jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumpokea atakapowasili na Taifa Stars.

"Tutakuwepo Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere pamoja na familia yake kwa maana ya mke na mtoto wake, tutakuwa na taji letu ambalo atamvisha mdogo wake aitwaye Sophia, hatujawahi kwenda kumpokea hii pia itakuwa ni mara yetu ya kwanza kumpokea Samatta akitoka nje, lengo ni kuendelea kumtia moyo kwa kitu alichokifanya kwa familia ni kitu kikubwa mno," alisema Mzee Samatta.

Mbali na tukio hilo, Mzee Samatta na familia yake pia wamepanga kumwandalia tafrija fupi endapo mtoto wao huyo kipenzi cha wanasoka nchini atakuwa na nafasi baada ya kumaliza majukumu ya Taifa Stars inayojiandaa na mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2018, mechi itakayochezwa Novemba 14, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

"Tutamwandalia tafrija fupi tu ya kumpongeza ila siwezi kuweka wazi kuwa itafanyika siku gani, na ndipo hapo tutakapompa kitu tulichomwandalia ambacho mpaka sasa bado ni siri yetu, hiyo itategemea na nafasi yake atakayokuwa nayo baada ya mechi ya Stars," alisema.

SAMATTA AMLIZA BABA YAKE
Waandaaji wa michuano hiyo walipotangaza kuwa Samatta ndiye Mfungaji Bora kwenye michuano hiyo, Mzee Samatta alitokwa na machozi ya furaha kwa kile alichodai kuwa wakati yeye akicheza hakuwa kufikia hatua hiyo kutokana na baadhi ya watu kumfanyia 'figisufigisu'.

"Nilitokwa na machozi ya furaha kusikia hivyo, rafiki zangu wengi walinipigia simu kunipongeza, Samatta amenipa faraja ya moyo ambayo niliumia wakati mimi nacheza kwani sikuweza kufikia hatua yake kutokana tu na baadhi ya mambo ya watu kwenye soka.

"Machungu niliyokuwa kuwa nayo sasa yamefutwa na mwanangu Samatta, nampongeza sana kijana wangu na ninaamini atafika mbali zaidi," alisema Mzee Samatta.


Mbali na kutwaa tuzo hiyo, Samatta ambaye huvaa jezi namba 10 akiwa Stars iliyokuwa inavaliwa na baba yake wakati huo anacheza Simba na Taifa Stars ambako kote Samatta amepita, ameingia kwenye kinyang'anyiro kingine cha kuwani tuzo ya Mwanasoka Bora anayecheza soka katika Klabu za Afrika ambazo fainali zake zitafanyika Januari nchini Nigeria.

Post a Comment

 
Top