BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda aliyekuwa Lubumbashi.
MFUNGAJI Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Mbwana Samatta amepanga kwenda nyumbani kwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kwa ajili ya kumpongeza kwa kumaliza kipindi chake cha uongozi huku akitumia nafasi hiyo kumpatia zawadi ya jezi namba tisa aliyoitumia kwenye mchezo wa fainali ya ligi hiyo iliyochezwa juzi Jumapili jijini Lubumbashi. 


Samatta ataongozana na straika mwenzake wanaocheza wote TP Mazembe ya DR Congo, Thomas Ulimwengu kwa pamoja watamuonyesha Kikwete medali za dhahabu walizopewa baada ya kutwaa ubingwa huo na kumkabidhi jezi kama kumbukumbu yake.


"Nimeona nimpe zawadi ya hii jezi Mheshimiwa Kikwete kwa mchango wake kwenye michezo na sapoti aliyotupatia sisi na wanamichezo wengine,'' alisema Samatta.


Kikwete anakumbukwa na jamii ya wanamichezo kwa jitihada zake za kukuza na  kuendeleza michezo huku akiwaweka karibu  wanamichezo na wasanii.Samatta na Ulimwengu wanatarajia kutua jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kulitetea taifa lao kwenye mechi ngumu dhidi ya Aljeria ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2018 mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja Taifa, siku ya Jumamosi.

Post a Comment

 
Top