BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi 'Mido'
SIMBA leo imecheza mechi ya kirafiki na timu yao ya vijana 'Simba B' na kuibuka na ushindi wa bao 2-0, mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.


Winga Brian Majegwa ndiye aliyeanza kuipatia Simba bao la kwanza dakika ya pili tu tangu mpira uanze akiunganisha krosi iliyopigwa na Emery Nimubona.
Dakika ya 15, mshambuliaji Hija Ugando anayefanya majaribio na kikosi cha Simba akitokea Kenya, alikosa bao la wazi baada ya kubaki yeye na nyavu baada ya kuwapiga chenga mabeki wawili na kipa wa Simba B lakini alishindwa kufanya maamuzi ya haraka kipa akarudi na kuucheza kwa mguu ukatoka ikawa kona ambayo haikuzaa matunda.

Hija Ugando


Baada ya mapumziko ya dakika nane, timu hizo zilirudi uwanjani huku zote zikionyesha kujipanga ingawa Simba B walitengeneza nafasi za kufunga lakini tatizo lilionekana ni kutokuwa makini katika umaliziaji.

Hata hivyo, Simba B walionekana kuzidiwa ujanja na kaka zao kwani wachezaji Joseph Kimwaga na Peter Mwalyanzi walionekana kuwachezea watakavyo ambapo dakika ya 80, Ugando aliifungia Simba bao la pili kwa shuti kali baada ya kugongeana vyema mpira na Mwalyanzi.

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo, Kocha wa Simba, Dylan Kerr aliwataka wachezaji wake Issa Said, Danmy Lyanga, Abdi Banda na Ugando anayefanya majaribio akitokea timu ya Nakuru ya Kenya
kuwa wanatakiwa kuongeza juhudu kwenye kikosi chake.


"Nilitaka kuangalia uwazo wa mchezaji mmoja mmoja maana kuna baadhi walikuwa ni majeruhi wa muda mrefu kama Mohamed Fakhi, hivyo nawataka wachezaji kuongeza juhudi zaidi watambue kama wapo kwa ajili ya kuisaidia Simba kwa kila hali,'' alisema Kerr huku akiweka wazi kuwa Ugando bado yupo chini ya uangalizi.

Kwa upande wa Ugando alisema ''Hapa nafanya majaribio ya wiki moja kuna ushindani mkubwa ndani ya Simba lakini napambana kuonyesha uwezo wangu kwani najiamini kuwa naweza,''.

Kerr aliwapa nafasi ya kucheza wachezaji wake wote waliokuwepo kwenye mechi hiyo.

Post a Comment

 
Top