BOIPLUS SPORTS BLOG

 Stars mazoezini leo
TAIFA Stars inatarajia kucheza mechi ya kirafiki Jumapili na timu ya Chuo Kikuu cha Pretoria (Tucks FC) jijini Johannesuburg ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Algeria Novemba 14, utakaochezwa jijini Dar es salaam.

Mchezo huo wa kirafiki ni sehemu ya progamu ya kocha mkuu, Charles Mkwasa baada ya kufanya mazoezi na vijana wake kwa siku nne mpaka sasa, anahitaji kuona maendeleo ya kikosi chake kabla ya kurejea nyumbani kwa mchezo dhidi ya Mbweha wa Jangwani Algeria.

Stars iliyowasili jijini Johannesburg Jumatatu mchana, imefikia katika hoteli ya Holiday Inn Express iliopo eneo la Woodmead ambapo imekuwa ikifanya mazoezi yake asubuhi na jioni katika viwanja vya St. Peters College na kituo cha cha michezo cha Edenvale.

Kuhusu hali ya kambi, Mkwasa amesema kuwa maendeleo ya wachezaji ni mazuri na wapo katika hali nzuri hakuna majeruhi na wanaendelea na maandalizi yao kama kawaida.

"Lengo la kuweka kambi huku ni kupata nafasi ya kuwaandaa vijana kwa mazoezi katika mazingira mazuri ikiwamo viwanja vya mazoezi, chakula na malazi kinachopelekea kuongezeka kwa umakini katika mazoezi.

"Tumeanza na mazoezi ya kujenga utimamu wa mwili kwa wachezaji, nguvu na stamina, pumzi ili kuhakikisha vijana wote wanakuwa katika kiwango sawa (fitness level) kisha tutaendelea na mazoezi ya kiufundi kwa siku zilizosalia kabla ya kurejea nyumbani," alisema Mkwasa.

Wachezaji 26 waliopo kambini ni magolikipa Ally Mustafa, Aishi Manula na Said Mohamed, walinzi ni Shomari Kapombe, Juma Abdul, Ramadhan Kessy, Mohamed Hussein, Mwinyi Haji, Hassan Isihaka, Salim Mbonde, Kelvin Yondani na nahodha Nadir Haroub “Cannavaro”.

Wengine ni Himid Mao, Frank Domayo, Mudahir Yayha, Salum Abubakar, Said Ndemla, Jonas Mkude, Salum Telela, Farid Musa, Saimon Msuva, Malimi Busungu, Elias Maguri, John Bocco na Mrisho Ngasa.

Aidha wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea klabu ya TP Mazembe ya Congo DR, wanatarajiwa kuungana na kikosi cha Stars baada ya mchezo wao wa fainali Ligi ya Mabingwa Afrika Jumapili dhidi ya USM Algiers.

Post a Comment

 
Top