BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Blida, Algeria
TIMU ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' usiku huu imeondolewa kwenye michuano ya kuwania kufuzu kwa kombe la Dunia 2018, baada ya kukubali kichapo cha mabao 7-0 ilipopambana na Algeria jijini Blida hivyo kuwa imeondolewa kwa jumla ya mabao 9-2.

 Katika sekunde ya 40 tu Algeria walifika langoni mwa Stars kwa Islam Sliman kupiga krosi safi iliyomkuta mshambuliaji wa FC Porto, Yacine Brahimi aliyeuweka mpira wavuni.


Bao hili lilitokana na wachezaji wa Stars kujisahau kuwa wameshaingia mchezoni. Baada ya bao hilo Algeria waliendelea kuliandama lango la Stars huku ikionekana wazi  kuwa alihitajika kiungo mmoja zaidi kwenye eneo la kati la Stars kwavile mipira mingi iliyokuwa ikiokolewa na walinzi wake iliishia kwenye himaya ya Algeria.

Brahimi aliendelea kuisumbua ngome ya Stars na safari hii kiungo wa Stars, Mudathir Yahya akiamua kumfanyia madhambi na kuambulia kadi ya manjano huku pia ikitolewa adhabu ndogo ambayo ilipigwa kiufundi na mlinzi wa kushoto wa Algeria na Napoli ya Italia, Faouz Ghoulam mpira uliotinga moja kwa moja nyavuni na kuiandikia Algeria bao la pili katika dakika ya 23.

Nusura Mbwana Samatta aipatie Stars bao kwenye dakika ya 26 baada ya kipa wa Algeria M'bolhi Rais kuanzisha mpira mfupi uliomkuta Samatta ambaye alipiga mpira dhaifu.

Katika dakika ya 40 mwamuzi wa mchezo huo alimzawadia kadi ya pili ya njano na kisha nyekundu Mudathir baada ya kumfanyia madhambi Brahimi.

Dakika tatu kabla ya mpira kwenda mapumziko, Riyad Mehrez aliipatia Algeria bao la tatu kwa shuti kali lililomuacha Barthez akiwa hana la kufanya.

Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha wa Stars Charles Mkwassa kufanya mabadiliko kwa kuwapumzisha Barthez na Farid Mussa huku nafasi zao zikichukuliwa na Aishi Manula na Salum Telela ambapo dakika mbili tu baada ya mabadiliko hayo, nahodha Nadir Haroub alifanya madhambi ndani ya eneo la hatari hivyo kusababisha penati na yeye akizawadiwa kadi ya njano. Penati hiyo ilipigwa na Islam na kuiandikia Ageria bao la nne.

Katika dakika ya 57 nahodha wa Algeria, Carl Medjani aliingia kwenye eneo la hatari lakini akafanyiwa madhambi na kipa Manula ambapo mwamuzi alitoa kadi ya njano kwa Manula na adhabu ya penati iliyopigwa na Fouz na kuifanya Algeria iongoze kwa mabao 5-0 hadi dakika ya 58.

Kwenye dakika ya 71, Manula alifanya kazi ya ziada kuokoa michomo miwili ya haraka haraka kabla mabeki hawajaokoa na kuwa kona iliyozaa bao la sita lililowekwa nyavuni kwa kichwa na nahodha Medjan. 

Mpira wa adhabu ndogo uliopigwa kuelekea langoni mwa Stars kwenye dakika ya 74 ulitua kichwani mwa Islam aliyeipatia bao la saba Algeria.

Kwenye dakika za mwisho washambuliaji wa Stars wanaoichezea TP Mazembe ya DR Congo, Samatta na Thoma s Ulimwngu walikosa mabao ya wazi ambayo yangeweza kufuta machozi ya Watanzania.

Katika mchezo huo zilishuhudiwa kadi za njano 11 huku Stars walipata nane na Algeria tatu.

Post a Comment

 
Top