BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
TAIFA Stars leo imeshindwa kuutumia vema Uwanja wa nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Algeria. Mchezo huo wa kwanza wa kuwania kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Dunia 2018, ilichezwa katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika dakika ya pili tu ya mchezo Stars walifanikiwa kulifikia lango la Algeria na kufanya shambulizi kali ambalo liliwainua maelfu ya mashabiki waliojazana uwanjani kuipa sapoti timu yao.


Thomas Ulimwengu ambaye alikuwa akitumika kama mwanzilishi wa mashambulizi aliendelea kuisumbua ngome ya Algeria hasa beki Ghoulam Fouzi anayeichezea Napoli ya Italia. 

Stars iliendelea kuliandama lango la Algeria mfululizo kabla hawajashtukizwa na shuti dhaifu la Benfodil Isha alilopiga baada ya kufanikiwa kumtambuka mlinzi wa Stars, Nadir Haroub 'Canavarho' ambaye aliteleza.

Kazi nzuri ya viungo Mudathir Yahya na Himid Mao ambao walicheza kwa maelewano makubwa nusura izae bao baada ya Mbwana Samatta kutengewa pasi nzuri ambapo shuti lake kali liligonga mwamba wa goli na mpira kurudi uwanjani kabla haujaokolewa na walinzi wa Algeria.

Samatta kwa mara nyingine alishindwa kuipatia bao la kuongoza Stars baada ya shuti lake kuokolewa na mlinzi wa Algeria wakati kipa M'bolhi Rais akiwa ameshaanguka chini katika dakika ya 32. Shambulizi hilo lilifanyika kabla ya Rais kuokoa shuti la Samatta wakiwa wanatazamana.

Stars iliyoonyesha kukosa bahati tu katika kipindi cha kwanza ilikosa bao jingine kupitia kwa Farid Mussa kabla Elius Maguli hajawainua watanzania katika dakika ya 43 kwa bao safi la kichwa akimalizia krosi ya Haji Mwinyi aliyegongana vizuri na Farid.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Stars walitoka wababe kwa bao hilo moja huku wakiwa wamekosa mabao matano ya wazi.

Kipindi cha pili kilianza kwa Algeria kufanya mabadiliko ambapo nyota wao pekee katika kikosi cha kwanza anayecheza ligi ya ndani katika klabu ya Ban Yas, Belfodil Isha alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na straika wa Tottenham Hotspurs ya Uingereza Bentaleb Nabil.


Samatta aliuthibitishia umma kuwa alistahili kutwaa kiatu hicho cha dhahabu baada ya kukusanya 'kijiji' toka katikati ya uwanja na kupiga shuti kali lililokwenda moja kwa moja nyavuni na kuiandikia Stars bao la pili.

Makosa yaliyofanywa na Mwinyi kwa kupoteza mpira yaliigharimu Stars bao lililowekwa kimiani na straika wa Algeria Isliman Islam anayecheza soka la kulipwa nchini Ureno katika klabu ya Sporting Lisbon.

Wakati Stars wanatafakari bao hilo, walijikuta wakipigwa bao la pili mfungaji akiwa ni yule yule Islam akipitia upande wa kulia ambao Mwinyi alionyesha kukosa kujiamini baada ya kufanya kosa la kwanza.

Katika mchezo huo refa Keita Mahamadou aliwaonyesha kadi za njano Himid na Bentaleb Nabil kwa kufanya madhambi.

Kikosi cha Stars kitaondoka alfajiri ya kesho kwenda Algeria kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa marudiano utakaopigwa siku ya Jumanne.

Post a Comment

 
Top