BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
STRAIKA wa Gor Mahia na timu ya Taifa ya Kenya 'Harambee Stars' Michael Olunga leo ameisadia timu yake kupata pointi tatu katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2018 baada ya kuifunga Cape Verde bao 1-0, mechi hiyo ilichezwa jijini Nairobi, Kenya.

Olunga ni miongoni mwa wachezaji walioziteka akili za viongozi wa Simba kwenye usajili wa msimu huu hasa aliposhiriki Kombe la Kagame jijini Dar es Salaam na kuibuka Mfungaji Bora wa michuano hiyo.


Hata hivyo Simba walishindwa kunasa saini ya mchezaji huyo baada ya kuambiwa ana mipango ya kwenda kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini katika moja ya timu iliyokuwa imetoa ofa ya dola 100,000 huku Simba wao wakitaka kumchukuwa kwa bei chee.

Olunga ambaye kwenye Ligi Kuu ya Kenya (KPL) amekuwa mfungaji wa pili akifikisha idadi ya mabao 16 akitanguliwa na Mfungaji Bora Jesse Were wakati timu yao ya Gor Mahia ikitwaa ubingwa huo.

Harambee Stars ilipata bao hilo pekee dakika ya tisa ambalo wapinzani wao walishindwa kusawazisha kutokana na uimara wa ukuta wa Wakenya hao ambao wanatakiwa kuifuata Cape Verde na mechi hiyo ya marudiano inatarajia kuchezwa Jumanne ya wiki ijayo.

Post a Comment

 
Top