BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga ameachia madaraka na kumkabidhi Rais wa Shirikisho la Soka Sudan, Dr Jaffar Mutasim ambaye aliwamwaga wapinzani wake katika uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika leo jijini Addis Ababa, Ethiopia.


Tenga ambaye ni Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), ameongoza chama hicho kwa miaka nane tangu akiwa anashika madaraka hayo hapa nchini na sasa hakugombea kwenye uchaguzi huo uliofanyika katika hoteli ya Intercontinental mjini Addis Ababa, ambapo Mutasim amepata kura sita kati ya kumi za wanachama wote wa  CECAFA waliopiga kura hizo.

Mutasim amewapiga chini wagombea wengine ambao ni Mganda, Lawrence Mulindwa aliyepata tatu huku Rais wa Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA), Vincent Nzamwita akipata moja tu, Rais wa Shirikisho la Soka la Ethiopia, Juneydin Bashar yeye alijitoa dakika za mwisho.

Akizungumza mara baada ya uchaguzi huo, Mutasim alisema kuwa anaamini kuingia kwake madarakani atashirikiana vyema na viongozi wengine katika kuiendeleza CECAFA ikiwa ni pamoja na kukuza soka kwneye ukanda wa nchi hizo wanachama.

''Nashukuru kuwa Mwenyekiti wa CECAFA, naishukuru pia serikali ya Ethiopia kwa kutoa ushirikiano wao katika maandalizi ya michuano hii ya Challenji, tukishirikiana tunaweza kufanya kazi ili kufikia malengo tuliyokusudia kwa ukanda huu," alisema Mutasim 

Mkutano wa leo ambao hufanyika kila mwaka wakatika wa michuano hiyo, ulihudhuliwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Robert Asembo na wagombea nafasi ya urais ya FIFA, Jerome Champagne na Prince Ali pia walihudhuria.

Post a Comment

 
Top