BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Lubumbashi
HII sasa sifa, tiketi za kuingia Uwanja wa TP Mazembe kwenye mchezo wa fainali ya pili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika inayoandaliwa na CAF kati ya wenyeji TP Mazembe na USM Alger ya Algeria utakaopigwa kesho jijini Lubumbashi, zilianza kuuzwa jana saa mbili asubuhi na kumalizika baada ya masaa mawili tu.


Mazembe ambayo ndio timu inapendwa zaidi hapa DR Congo inatumia Uwanja wake ambao una uwezo wa kuingiza watu 20,000 tu ambao ni theluthi moja ya wale wanaoweza kuingia kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na BOIPLUS mmoja wa mashabiki waliokosa tiketi hizo alisema licha ya kujitahidi kufika mapema katika eneo maalumu la kuuzia tiketi lililopo katika uwanja huo, bado alishindwa kupata. 

"Nilikuja mapema ila foleni ilikuwa ndefu nikakosa kabisa, sijui nifanye nini na sitaki kukosa mechi hii". alisema huku akiwa na masikitiko makubwa shabiki huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Sai.

Shabiki mtanzania, Victor Lema akionyesha tiketi yake


Mwandishi wa BOIPLUS alijaribu kuulizia upatikanaji wa tiketi hizo kwa lengo la kujua endapo zinaweza kuuzwa na walanguzi kama inavyofanyika nchini Tanzania ndipo akakutana na mtu ambaye alikuwa akiziuza kwa bei ambayo ni mara tatu ya bei ya kawaida.

Tiketi inayouzwa kwa Francs 3,000 (Sh 7,000) inauzwa kwa Francs 9,000 (Sh 20,000), ile ya Francs 5,000 (Sh 10,000) inapatikana kwa Francs 15,000 (Sh 30,000). Na ile ya Francs 10,000 (Sh 23,000) hupatikana kwa Francs 30,000 (Sh 70,000).
Tiketi ambazo hazikupatikana ni za VIP ambazo huuzwa kwa Dola 500 ambayo ni zaidi ya Sh 1 milioni.

Post a Comment

 
Top