BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
KLABU ya TP Mazembe leo imeongeza uwezekano wa kubeba kombe la mabingwa wa Afrika baada kushinda ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya USM Alger. 

Licha ya USMA kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa, ni Mazembe ndio waliofanikiwa kuzitingisha nyavu za wenyeji kwenye dakika ya 27 baada ya Rainford Kalaba kuachia shuti kali akiwa nje ya eneo la 18 na kutinga nyavuni huku kipa wa USMA akichupa bila mafanikio. 


Bao hilo lilipatikana baada ya straika mtanzania Thomas Ulimwengu kumpa pasi maridadi mfungaji ambaye hakufanya ajizi.

Wakat timu zikikaribia kwenda mapumziko, Mazembe walipata pigo baada ya nyota wake Kalaba kulimwa kadi nyekundu baada ya kudaiwa kumsumkuma mlinzi wa USMA. Picha za marudio za video zilionyesha wazi mlinzi huyo alijiangusha.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku USMA wakionyesha wazi wanatafuta bao la kusawazisha. Hata hivyo umakini wa vijana hao wa Moise Katumbi ulizidi kuondoa uwezekano wa USMA kupata bao.

USMA nao walipata pigo baada ya mlinzi wao Hocine El Orfi kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kuushika mpira kwa makusudi ndani ya eneo la hatari. Mazembe walizawadiwa penati ingawa kiungo wa kutumainiwa, Sinkala alikosa penati hiyo baada ya kipa wa USMA kupangua shuti lake.

Mazembe waliendelea kuliandama lango la USMA na katika dakika ya 77 mtanzania Mbwana Samatta 'Poppa' aliitoka ngome ya USMA na kubaki akitazamana na kipa, lakini kabla hajafanya lolote mlinzi wa USMA alimfanyia madhambi na refa kuamuru ipigwe penati. Samatta aliukwamisha mpira huo wavuni na kuiandikia Mazembe bao la pili dakika ya 79.

USMA walipata bao lao la kufutia machozi kupitia kwa Seguer dakika ya 88 baada kupiga shuti kali lililomshinda Robert Kidiaba.

Mazembe wanaondoka Algeria wakiwa na matumaini tele ya kubeba kombe hili kwa maana katika mchezo wa marudiano utakaopigwa siku ya jumapili septemba 8, wanahitaji japo sare ya aina yoyote kubeba 'mdoo' hiyo wakiwa nyumbani DR Congo.

Post a Comment

 
Top