BOIPLUS SPORTS BLOG

TAIFA  Stars leo inaingia  uwanjani kumenyana na Algeria 'The Desert Worriors' katika mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika 2018 nchini Russia. Mechi itachezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mzunguko uliopita Stars iliitoa Malawi ingawa ilikuwa katika wakati mgumu. Mechi ya marudiano Kocha Mkuu wa Stars Charles Mkwasa alilazimika kuongeza kiungo mmoja wa kati na kuua winga moja, mfumo ambao ulisaidia kupata matokeo mazuri.


Makocha, wachezaji na mashabiki wanapaswa kukubali kwamba Algeria ni bora zaidi yetu. Kwa kuamini na kukubali hili mwalimu hatothubutu kupanga kikosi chenye viungo wawili wa kati hata kama Stars ipo nyumbani.

Mkwasa anatakiwa kuhakikisha ainaifunga Algeria kwa kupanga viungo wawili wakabaji ambao wanaweza kuwa Himid Mao na Salum Telela huku akiweka kiungo mmoja mshambuliaji ambapo kinda Said Ndemla ameonyesha uwezo mkubwa.

Kwa kutumia mfumo wa 4-2-3-1 Mkwasa anaweza kuwapa majukumu ya kushamabulia kwa kasi wakitokea pembeni mawinga Thomas Ulimwengu na Mrisho Ngassa au Farid Mussa huku nyuma ya straika Mbwana Samatta akisimama Ndemla.

Hakuna tatizo lolote katika safu ya ulinzi na kwamba Shomari Kapombe katika upande wa kulia amekuwa bora na kwasasa ni kama  hana mpinzani. Haji Mwinyi amefanikiwa kuuteka moyo wa mwalimu kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukaba na kupandisha mashambulizi huku kimo chake kikimsaidia kupambana na washamuliaji warefu.

Kuzoeana kwa walinzi wa Yanga Kelvin Yondan na Nadir Haroub 'Canavaro' inaweza kuwa ni faida nyingine kwa taifa letu kwenye mchezo wa leo. Uzoefu wao wa kupambana na washambuliaji wa aina mbalimbali ni sifa nyingine itakayomlazimu Mkwasa kuwapanga.


Katika kikosi cha Algeria kuna uwezekano kukawa na mchezaji mmoja tu anayecheza ligi ya ndani, wengine wote ni wachezaji wa kulipwa katika ligi kubwa barani Ulaya kama Ufaransa, Hispania, Uingereza, Ureno na Italy.

Lakini hii imeonyesha kuwa si tatizo kwa Mkwasa kwavile anajivunia mastraika Mbwana Samatta na Ulimwengu waliotoka kubeba kombe la ligi ya mabingwa Afrika wakiwa na TP Mazembe huku akikiri morali ya wachezaji na muitikio wa mazoezi ni mambo yanayompa matumaini makubwa.

"Timu ina morali ya hali ya juu, kila mchezaji anaonyesha hamu ya kuliwakilisha vema taifa lake, hii inanipa imani kubwa kuwa tutawashangaza waalgeria hapa. Nafurahi kuona wachezaji wanatekeleza yale ninayowalekeza, hii ni ishara ya ushindi,'' alisema Mkwasa

BOIPLUS inaungana na watanzania wote kuitakia kila la kheri Taifa Stars katika mchezo wa leo na inaamini watanzania wengi watajitokeza uwanjani kutoa sapoti kwa timu.

Post a Comment

 
Top