BOIPLUS SPORTS BLOG


KATIKA kile kinachoonekana kuwa Wakongo wamejiimarisha katika ulinzi kuelekea fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya TP Mazembe na USM Algers leo, vimewekwa vizuizi vingi vya kuingia mtaa wa Kamalondo ulipo Uwanja wa TP Mazembe.

Mamia ya polisi wa Usalama wamemwagwa mtaani huku wengi wakiwa wamekaa katika vizuizi maalumu vilivyotengenezwa kwa ajili ya ukaguzi wa watu wanaokwenda uwanjani hapa.


Katika vizuizi hivyo vilivyoanzia umbali wa mita mia nne kutoka uwanjani, polisi hukagua watu wote wanaokwenda na wale wenye tiketi tu ndio wanaoruhusiwa kuingia mtaa huu. Kwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hii ni sawa na kuweka vizuizi kuanzia maeneo ya CDS Club (zamani TCC Club, Chang'ombe) au Chuo cha Uhasibu (T.I.A) na kuwazuia wasio na tiketi wasisogee karibu na uwanja huo.

Mwandishi wa BOIPLUS alifanikiwa kuvuka kizuizi cha kwanza kwa kuonyesha kadi yake ya kuingilia uwanjani lakini alikwama kwenye kizuizi cha pili kutokana na kushindwa kuelewana lugha na Polisi ambao huzungumza Kifaransa na Kilingala tu wakati mwandishi yeye alikuwa akijieleza kwa lugha za kiswahili na kiingereza. Hiyo ilipelekea asubiri kwa dakika kadhaa hadi alipokuja askari ambaye anazungumza Kiswahili.


Baada ya hapo BOIPLUS ilizungumza na askari huyo na kumuuliza sababu za ulinzi wa hali ya juu hivyo ndipo ilipotolewa sababu ya ya matishio ya uvamizi wa vikundi vinavyopingana na serikali.

"Kuna vikundi vya kijeshi vinavyopingana na serikali, vinaweza kuleta shida kukiwa na mikusanyiko ya watu wengi, hivyo ni lazima tuwe waangalifu sana,".

BOIPLUS itaendelea kukuletea kila kinachojiri hapa, bonyeza www.boiplus.blogspot.com kila wakati ili kupata taarifa zote

Post a Comment

 
Top