BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi 'Mido'
VIJANA kutoka matawi mbalimbali ya Simba ya wilaya zote za jiji la Dar es Salaam wameonekana kuchukizwa na msuguano unaondelea ndani ya klabu hiyo ambayo wiki hii kocha msaidizi Seleman Matola alibwaga manyanga kwa madai kuwa hawezi kufanya kazi na bosi wake Dylan Kerr aliyesema ni mbishi.

Hayo yalisemwa katika kikao kilichoshirikisha vijana zaidi ya 50 kilichofanyika Ukumbi wa CDS Chang'ombe zamani TCC Club, jijini  Dar es Salaam huku lengo kubwa la mkutano huo ilikuwa ni kuundwa kwa Umoja wa Vijana wa Simba utakaoshirikisha matawi yote na vijana wote wa Simba kwa ujumla.


Kwa pamoja vijana walionyesha kutopendezwa na hali ya kuwepo kwa misuguano na kutoelewana kwa matawi au makundi mbalimbali ndani ya klabu hiyo hali ambayo wanaona inawapa tabu viongozi wao kuongoza timu kutokana na ukweli kwamba makundi yote hayashirikiani vyema na kutoa ushirikiano mzuri kwa uongozi katika kuleta maendeleo ya Simba.

Vijana hao wanaamini kuwa klabu yao  isipokuwa na umoja wa kweli kwa wanachama wote basi ni vigumu sana kupata mafanikio. Hivyo walitoa wito kwa wanachama wengine kuondoa tofauti zao na kushirikiana ili kuijenga Simba.

Mkutano uliazimia kwa pamoja kuundwa kwa umoja huo na kuwa na sauti moja ili kuijenga Simba ya baadae yenye umoja wa kweli kwa wanachama wote. Mkutano uliunda kamati ya muda itakayosimamia mchakato wa kuundwa kwa umoja huo. Kamati hiyo itakuwa kama ifuatavyo;

1. Mwenyekiti - Mathew Kawogo
2. Makamu M/kiti - Abeid King
3. Katibu - Ayoub Simba
4. Katibu Msaidizi - Severin Machila
5. Mweka Hazina - Alfeji Kehongo
6. Msemaji - Ally Masaninga
7. Wajumbe
Fihi Kambi
Frank Pojo
Shaban Hemed
Siraji Rashid
Mohammed Nammenge
Geffrey Shimwela
Ibrason Isack
Mwarami Ngatanda
Said Kipende


Majukumu ya kamati yatakuwa; 
1. Kuandaa kanuni mbalimbali za umoja wa vijana
2. Kushawishi vijana kujiunga na umoja wa vijana ili kuwaunganisha na kuwa kitu kimoja.
3. Kuandaa na kuitisha mkutano wa vijana.

Mkutano umeazimia kuwa kamati hiyo ipewe muda wa miezi mitatu tu kukamilisha kazi waliyopewa huku vijana hao wakiwataka viongozi wao kutafakari kwa kina suala la kumpatia nafasi Mohammed Dewji 'MO' ya uwekezekaji katika timu. 

Post a Comment

 
Top