BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
KLABU Bingwa ya Afrika, TP Mazembe ya DR Congo itaondoka kesho jumatatu nchini humo kuelekea Japan  inakokwenda kushiriki michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia ambapo Barcelona ya Hispania italiwakilisha bara la Ulaya.


Mazembe ambayo ina watanzania wawili Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, ambao wameweka rekodi ya kuwa watanzania wa kwanza kubeba kombe la Mabingwa Afrika, inaelekea Japan ikiwa na ari kubwa kutokana na ubingwa walioutwa mbele ya Timu ngumu ya USM Alger ya Algeria katika fainali iliyopigwa jijini Lubumbashi Novemba 8.

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Disemba 10 na kumalizika Disemba 20 katika Uwanja wa Yokohama huku  ikihusisha mabingwa wa mabara mengine wakiwemo Barcelona, Club America, River Plate, Auckland City na klabu moja ambayo itashinda na kupata uwakilishi kutoka kwenye ligi ya Japan.


Vijana hao wa Tajiri Moise Katumbi watapitia nchini Ethiopia ambako watalala kwa siku moja kabla hawajaondoka kwenda Japan kwa kupitia Goungzhou, China.

BOIPLUS inawatakia kila la heri watanzania Samatta na Ulimwengu katika michuano hiyo ili waweke rekodi nyingine ya kuwa watanzania wa kwanza kutwaa kombe la Klabu Bingwa ya Dunia.

Post a Comment

 
Top