BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
MSHAMBULIAJI Emanuel Mtumbuka aliyekuwa kwenye mipango ya Kocha wa Simba, Dylan Kerr leo aliifungia bao Polisi Tabora katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga ambapo walitoka sare ya bao 1-1.

Mtumbuka ambaye yupo katika hatua za mwisho za usajili katika kikosi hicho kilicho chini ya kocha Richard Amatre aliipatia bao hilo la kuongoza kabla ya nahodha wa Mwadui, Bakari Kigodeko kusawazisha bao hilo.


Katika usajili mkubwa wa Ligi Kuu Bara, Mtumbuka alijiunga na Simba ambao walimpa nafasi ya kufanya majaribio huku Kerr akiridhishwa na kiwango chake na kuwataka viongozi wa Simba kumpa mkataba lakini jambo hilo lilionekana kuwa gumu kukamilika kwa upande wa viongozi hao.

Pamoja na sare hiyo, Mtumbuka alifanikiwa pia kutoa pasi nyingi kwa wenzake lakini hazikuzaa matunda kutokana na umaliziaji mbovu. Jana Polisi Tabora walicheza na Stand United kwenye Uwanja huo wa Ally Hassan Mwinyi na kufungwa bao 2-0.

Mtumbuka ambaye anamudu vizuri kucheza winga zote mbili, mshambuliaji wa pili pamoja na kiungo mshambuliaji ameonyesha kuwavutia pia Acacia Stand United na Polisi Moro.

Endapo mshambuliaji huyo atasaini mkataba na timu hiyo yenye maskani yake mjini Tabora basi ataweza kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho kinachopambana kupanda daraja kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Post a Comment

 
Top