BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
KIUNGO wa Simba, Awadh Juma hayupo kambini na wenzake. Iko hivi, tangu mchezaji huyo arejee nchini akitokea kwenye majukumu ya timu ya Taifa 'Kilimanjaro Stars' hakwenda visiwani Zanzibar kwani mkataba wake na Simba umemalizika.


Alichokifanya Awadh ni kuwaweka wazi viongozi wake kwamba apewe mkataba wa mwaka mmoja tu ndipo atajiunga na kikosi hicho jambo ambalo lilianza kushughulikiwa na kesho au kabla ya Jumamosi atakuwa amepewa mkataba huo.

Awadh amesema kuwa ameamua kuchukuwa mkataba wa mwaka mmoja kwasababu anaweza kuwa na mambo mengine ya kufanya ama kujitokeza na akashindwa kuyafanya kutokana na kubanwa na mkataba wa muda mrefu.


"Ni kweli sipo kambini na nipo Dar es Salaam, mkataba ulikwisha na sikuongezwa mwingine, hivyo ninataka nipewe kwanza mkataba ndipo nikafanye kazi ili nijue kuwa nipo chini ya nani kuliko kuwepo kwenye timu bila mkataba. Nilikuwa na majeraha kidogo nilipotoka Ethiopia ila si ya kunizuia kwenda Zanzibar kwani nilianza kufanya mazoezi mepesi ya peke yangu.

"Tulifanya mazungumzo ambayo yamekwenda vizuri na leo nilitakiwa kusaini mkataba huo ila sijafanya hivyo kutokana na sababu tofauti lakini naamini kama sio kesho basi kabla ya mechi ya Jumamosi nitakuwa nimesaini japokuwa sitaweza kucheza mechi hiyo kwani sijafanya mazoezi na wenzangu," alisema Awadh

Post a Comment

 
Top