BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
AZAM FC imeutumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Chamazi kwa kuifunga Kagera Sugar bao 2-0 katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara hivyo kuifanya Azam ifikishe pointi 32 nyuma ya Yanga inayoshika usukani ikiwa na pointi 33.


Kipre Tchetche ndiye aliyekuwa wa kwanza kuipatia bao Azam katika dakika ya tisa baada ya kuunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Himid Mao na yeye akimalizia kwa kichwa.

Baada ya bao hilo, Kagera Sugar waliongeza juhudi ambapo walifanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Azam lakini umakini wa kipa Aishi Manula uliwasaidia Azam kuzuia mabao hayo.

Dakika ya 35, Kagera Sugar walipata penati ambayo ilipigwa na beki Salum Kanoni lakini Manula alifanikiwa kupangua penati hiyo na kusababisha kona ambapo Kanoni alipiga kona mbili ambazo hazikuzaa matunda.

 
Mwamuzi wa mchezo huo alitoa kadi kwa Azam, Himid Mao na Salum Abubakar 'Sure Boy' baada ya kucheza rafu kwa wachezaji wa Kagera Sugar huku Shaban Ibrahimu na Daudi Jumanne nao wakipewa kadi kwa kuwachezea rafu wachezaji wa Azam.

Timu hizo zote zilicheza kwa kushambuliana lakini Azam ilionekana kuzidiwa kwani Kagera Sugar walipata nafasi nyingi za kufunga lakini kutokuwa makini kwa washambuliaji wa Kagera kuliwanyima mabao hayo.

Makocha wa timu zote mbili walifanya mabadiliko ambapo Stewart Hall aliwatoa John Bocco, Michael Balou nafasi zao zilichukuliwa na Farid Musa pamoja na Ramadhan Singano 'Messi' huku kocha Adolf Rishard akimtoa Paul Ngway nafasi yake ilichukuliwa na Adam Kingwande.

Uzembe wa mabeki wa Kagera Sugar uliwagharimu dakika ya 73 ambapo walimuacha kiraka wa Azam, Shomari Kapombe kwenda kucheka na nyavu zao.

Post a Comment

 
Top