BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Chamazi
BAO pekee la straika wa Azam FC, John Bocco limetosha kuishusha Yanga kileleni kwa kufikisha pointi 35 huku Yanga wakiwa na pointi 33 hivyo kuipeleka hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.


Issa Rashid 'Baba Ubaya' kulia akihakikisha Didier Kavumbagu haleti madhara langoni mwa Mtibwa

Mtibwa Sugar ambao wamekubali kichapo hicho kwenye uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam wamebaki nafasi ya tatu wakiwa na pointi 27 nafasi ambayo pia inawaniwa na Simba wanaoshika nafasi ya nne kwa kukusanya pointi 24 na keshokutwa Ijumaa wana mechi dhidi ya Ndanda.

Mechi hiyo itakayopigwa uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara ndiyo itaamua kama Simba wataishusha Mtibwa ama watashindwa.

Bocco alipata bao hilo dakika ya 87 baada ya kupiga faulo nje kidogo ya 18 ikiwa ni faulo iliyotokana na yeye kuangushwa na mchezaji wa Mtibwa Sugar.

Mtibwa Sugar ilicheza mpira kwa kujiamini huku wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Azam ingawa mashambulizi yao hayakuzaa matunda huku Azam wakitumia faulo hiyo moja kupata pointi tatu.Makocha wote walifanya mabadiliko ambapo kocha wa Azam, Stewart Hall aliwatoa Frank Domayo, Didier Kavumbagu na Farid Musa nafasi zao zilichukuliwa na Mudathir Yahaya, Kipre Tchetche na Ramadhan Singano.

 Kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime naye aliwatoa Said Bahanuzi, Boniface Maganga na Mohamed Ibrahim nafasi zao zilichukuliwa na Jaffar Salum, Shaban Nditi na Ibrahim Rajabu.

Hata hivyo mchezo huo ambao ulikuwa na upinzani mkubwa ulisababisha wachezaji wapate kadi ambapo Mwamuzi Ngole Mwangole alitoa kadi za njano kwa wachezaji wa Mtibwa Sugar, Henry Joseph, Nditi na Said Mohamed wakati Jean Mugiraneza 'Migi' naye akipewa kadi hiyo ya njano.

Azam na Mtibwa kwasasa zinajiandaa na mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambapo zimepangwa kundi moja na Yanga.

Post a Comment

 
Top