BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
YANGA imemtupia virago kiungo wao Haruna Niyonzima kwa kile kinachoelezwa ni kuchoshwa na tabia za utovu wa nidhamu wa mchezaji huyo raia wa Rwanda ambazo zimekuwa zikiiathiri timu yao na kwamba anatakiwa kulipa dola 71,175 ambazo ni zaidi ya Sh 149 milioni.


Hata hivyo, Niyonzima amesema kuwa bado ni mchezaji wa Yanga mpaka pale watakapompa barua ya kuvunja mkataba wake kwani mpaka leo hii walipotangaza kuvunja mkataba wake hakuwahi kupewa barua yoyote ikiwemo ile ya kusimamishwa kwa muda usiojulikana.

Niyonzima alisema kuwa anachokifahamu yeye kutoka kwa viongozi wa Yanga ni kutakiwa kupeleka vielelezo vya matababu ya mguu aliyokuwa akiyapata akiwa na timu yake ya Taifa ya Rwanda iliyoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji nchini Ethiopia.

Niyonzima alisema kuwa leo alifika makao makuu ya Yanga na kumkabidhi vielelezo hivyo Katibu mkuu, Jonas Tibohora ila cha ajabu alipokabidhi aliambiwa kuwa tayari wametangaza kuvunja mkataba wake na yeye hakukabidhiwa barua ya kuvunjwa kwa mkataba huo.

''Hata mimi nimesikia kuwa mkataba wangu umevunjwa. Nilienda pale lakini sikupewa barua yoyote ambayo mimi naweza kuisoma na kuitolea ufafanuzi ila ninachoweza kusema kwasasa ni kwamba kama watanipa barua nitaisoma na kuangalia vigezo walivyotumia kuvunja mkataba.

''Kama kuna mahali natakiwa kuwalipa na mkataba kama unasema hivyo basi nitawalipa ila hili nitalitolea ufafanuzi nikipewa hiyo barua kwa sasa nina msongo wa mawazo kwani hili jambo lililonitokea si dogo ni kama pale mfanyakazi yoyote anapoachishwa kazi ghafla,'' alisema Niyonzima.

Kuhusu kusumbuliwa na mguu alisema kuwa ''Niliumia mguu tangu mwaka jana na hili viongozi wa Yanga wanalifahamu na niliamua kujitibu mwenyewe na mpaka nilifanya hivyo kuna sababu kati yangu na wao ila nilijitibu kwa vile mpira ndiyo ajira yangu.

''Hayo ni maneno tu ya watu, mimi sina mapenzi na Simba kama ni mapenzi ya timu basi ningeipenda APR ambayo imenilea kisoka mpaka Yanga wakaniona mimi huwa nakuwa na mapenzi na timu ninayofanyia kazi na hakuna kitu kama hicho kuwa ni utovu wa nidhamu,'' alisema Niyonzima

Niyonzima alisema kuwa kwasasa bado hajaamua afanye nini na uamuzi wake utatoka pale atakapopewa barua na hata kama hatabaki anaamini bado anaweza kucheza sehemu nyingine na nchi yoyote iwe Tanzania ama nje ya hapa.

''Ninachosikitika ni kutoa uamuzi pasipo kukaa na mimi, nimeichezea Yanga kwa miaka mitano lakini sasa hawaoni hata zuri langu, wamenisikitisha na kunifedhehesha sana lakini yote hii ni mipango ya Mungu,'' alisema

Yanga wamempiga kitasa mchezaji huyo kuwa hataweza kusajiliwa popote mpaka alipe fedha hizo ama timu itakayomuhitaji imlipie.

Post a Comment

 
Top