BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
KIPA wa Mtibwa Sugar, Hussein Shariff 'Casillas' yupo Afrika Kusini kwa ajili ya majaribio ya wiki mbili na timu ya Royal Eagles anayochezea Uhuru Seleman kwa mkopo akitokea Jomo Cosmo.

Casillas amekwenda kujaribu bahati yake na akifanikiwa majaribio hayo basi atakuwa amepata shavu kuichezea timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini humo.


Kwa mantiki hiyo, Royal Eagles kama itaridhika na kiwango cha kipa huyo watalazimika kufanya mazungumzo na Simba ambao ndiyo wamiliki halali wa Casillas kwani Mtibwa Sugar anacheza kwa mkopo baada ya kukosa nafasi kwenye kikosi hicho cha Msimbazi.

Kocha wa makipa wa Mtibwa Sugar, Patrick Mwangata amethibitisha kuondoka kwa kipa huyo na kwamba atarejea baada ya wiki mbili huku akiamini kwamba kipa wao atafanya vizuri.

''Ni kweli amekwenda kujaribu bahati yake Afrika Kusini. Mungu akimsaidia atafanikiwa kile anachokihitaji, Casillas ni kipa mzuri ila majeraha ndiyo yaliyomrudisha nyuma ingawa kwasasa amepona kabisa,'' alisema Mwangata

Casillas aliamua kwenda Mtibwa kwa mkopo baada ya kuumia ugoko wa mguu na hivyo kushindwa kucheza kwa muda mrefu ambapo msimu uliopita Simba walikuwa wakimtumia zaidi Ivo Mapunda na Peter Manyika Jr.

Post a Comment

 
Top