BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
WEUPE wa jiji la Madrid, Real Madrid, leo wameutumia vema uwanja wao wa nyumbani, Santiago Bernabeu baada ya kuitandika Rayo Vallecano mabao 10-2 katika mchezo wa ligi ya Hispania 'La Liga'


Madrid walipata bao lao la kwanza mapema dakika ya tatu lililofungwa na mlinzi wa kulia Danilo kabla Antonio Amaya haijaisawazishia Rayo dakika saba baadaye.

Rayo walicharuka na kufunga bao la pili katika dakika ya 12 safari hii likifungwa na Jozabed. Furaha ya bao hili haikudumu kwavile dakika tatu tu baadae Rayo ilipata pigo baada ya mchezaji wake Tito aliyetoa pasi ya bao lao la pili, kupewa kadi nyekundu.


Gareth Bale aliisawazishia Madrid katika dakika ya 24 kabla Rayo haijapata pigo jingine katika dakika 28 baada ya mlinzi wake Jose Raul Baena kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano baada ya kufanya madhambi ndani ya eneo la penati. Mwamuzi alitoa adhabu ya penati iliyopigwa na Cristiano Ronaldo na kuiandikia bao la tatu Madrid.

Baada ya Rayo kupungukiwa na wachezaji wawili ilikosa kabisa nguvu ya kuendelea kupambana hivyo kuipa Madrid nafasi ya kuendelea kufunga mabao ambapo dakika 41 Bale aliifungia bao la nne.


Kipindi cha pili Madrid ilitawala zaidi mchezo na kuendeleza karamu ya mabao safari hii yakiwekwa kimiani na Benzema aliyefunga matatu, Ronaldo aliyeongeza moja na Bale aliyeongeza mawili na kufanya awe amefunga mabao manne peke yake katika mchezo huo.

Post a Comment

 
Top