BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
MAPEMA wiki hii timu ya Simba ambayo ipo jijini Mwanza kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ijayo dhidi ya Mwadui FC ilicheza mechi ya kirafiki na timu ya Daraja la Kwanza, Geita Gold Mine ambayo ipo chini ya aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola

Matola alijiuzulu kumsaidia Kerr  kwa kile kilichodaiwa kuwa Kerr hapendi kupewa ushauri jambo ambalo lilimfanya kazi yake kuonekana ngumu kwani ilifikia hatua walirushiana maneno mazito.

Katika mechi hiyo ya kirafiki ambayo kwa mujibu wa Kerr ilikuwa ni kwa ajili ya kuwaangalia wachezaji wake ambao hawapewi nafasi kama watamfaa kuwatumia kwenye mechi zijazo, Simba ilifungwa bao 3-1. Mechi hiyo ilichezwa mjini Geita.Baada ya mechi hiyo kumalizika na kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana, waandishi waliokuwepo hapo waliamua kuomba msaada wa kupanda basi la Simba lililokuwa limewabeba wachezaji na walikubaliwa kibinadamu tu ingawa taratibu haziruhusu, cha ajabu ni kwamba baada ya kupanda basi hilo, meneja wa Simba, Abbas Ally alianza kumshambulia mpiga picha wa BOIPLUS kwa maneno makali huku akimtaka ashuke haraka sana.

Sababu kubwa ya Abbas kufanya hivyo ni madai yake kwamba mpiga picha  huyo aliandika habari kuwa Kerr alikwenda disko na kulewa usiku pamoja na wachezaji jambo ambalo halina ukweli wowote na halijawahi kuandikwa kwenye chombo chetu bali ni taarifa ya chuki iliyopandikizwa na meneja huyo kwa benchi la ufundi.

Hilo halikuwa tatizo kubwa sana, kwani kukubali kuwapa msaada ama kukataa ilikuwa ni juu yao lakini si kupandikiza chuki kwa taarifa ambayo si ya kweli, waandishi hao walilazimika kushuka kwenye gari hilo na kutafuta usafiri mwingine wa kuwarudisha Mwanza kwavile waliona si busara wamuache peke yake mwandishi mwenzao. Yote ni kheri.Leo asubuhi mpiga picha wetu huyo huyo ambaye ameweka kambi jijini Mwanza maalumu kwa ajili ya kuripoti habari za Simba ikiwemo michezo yao miwili ya kanda ya ziwa, alikwenda kwenye mazoezi ya Simba, lakini cha kushangaza ni kwamba alipofika tu, Kerr alimvaa mwandishi huyo na kumkunja huku akitaka kupigana naye na lengo kuu ni kutaka atoke nje ya uwanja na wala asipige picha za mazoezi hayo.

Mbali na hilo, benchi la ufundi la Simba lilienda mbali sana kwa kumnyang'anya kamera mpiga picha huyo ambayo ilipokonywa na kocha wa makipa, Idd Salum bila kujuwa walikusudia kufanya nini juu ya kamera hiyo ingawa mtunza vifaa wao, Mtambo aliwasihi wasifanye chochote na kamera hiyo ndipo wakamrejeshea. 

Mpiga picha huyo hakuwa na hiana, baada ya purukushani hizo alitoka nje pasipo kufanya lolote huku akimkabidhi kamera yake mwandishi mwingine ambaye pia aliamuriwa aiweke ndani ya begi ilimradi tu BOIPLUS isichukue matukio yoyote uwanjani hapo huku wapiga picha wengine wakiendelea na kazi yao kama kawaida.

Wakati yote hayo yakiendelea wachezaji na watu wengine waliokuwepo ndani ya uwanja huo walibaki wakishangaa hasa kwa kitendo cha Kerr na kocha wa makipa kumfanyia fujo mpiga picha huyo ambaye kiukweli hakuwa na kosa na hakuna sehemu yoyote aliyoandika habari hiyo inayodaiwa kuandikwa kwenye chombo hiki.Baada ya kupata taarifa hizi za manyanyaso aliyoyapata mwandishi wetu niliona nisiendelee kukaa kimya. Ni vema nikatumia nafasi hii kumweleza Abbas kuwa BOIPLUS haijawahi kuandika habari ya Kerr na wachezaji kwenda disko usiku na kulewa. Na kama Abbas una ushahidi basi nakushauri uuweke wazi. Ila kama ulisimuliwa tu na huna ushahidi wowote basi nakusihi uache mara moja kumnyanyasa na kumzuia mwandishi huyo kufanya kazi yake. Ukumbuke kwamba kuna maisha mengine baada ya Simba kwani wengi walipita hapo na sasa hawapo na huwa wanakutana na sisi mtaani.

Kama kocha anafanya starehe hayo ni maisha yake binafsi, kikubwa afanye kazi iliyomleta Simba. Nimesikitika sana kuona mtu kama Kerr nae anakurupuka na kuanza kumyayasa mwandishi eti tu kwavile kasimuliwa hadithi na Abbas ambaye naamini na yeye amesimuliwa pia, nilitarajia Kerr kwa uweledi angetaka kwanza kuiona hiyo stori halafu aombe kuzungumza na mwandishi ili amweleze alikozipata taarifa hizo. Mwisho wa tabia hii ya ukurupukaji katika kufanya maamuzi ni kuanza kupewa habari zenye chuki na fitina na kuanza kubagua hata wachezaji.

Nathubutu kusema kwa umeneja wako huu Abbas ni wazi wanasimba na wadau wa soka wataanza kumkumbuka Nico Nyagawa ambaye licha ya kuwa alicheza mpira klabuni hapo kwa miaka mingi, alikuwa kiongozi mwenye hekima na busara na katika kipindi chake hatukuwahi kusikia malalamiko ya aina hii.
Meneja wa timu ana majukumu mengi sana, nashangaa Abbas unapata wapi muda wa kukaa na watu na kuanza kusikiliza hadithi zisizo na kichwa wala miguu huku ukisahau kuwa hao hao ndio watakaokucheka kesho ukiwekwa pembeni.

 Naamini kwa kutumia busara zako, utajutia alichomfanyia mwandishi aliyefunga safari toka Dar na kuweka kambi Mwanza wiki nzima kwa ajili ya Simba kama ambavyo Kerr ameonyesha kujutia kitendo alichokifanya leo huku akikiri kuwa amepewa taarifa ambazo si sahihi. Kama Kerr amegundua ulimdanganya basi thamani yako kwake itashuka pia. Kumbuka kwamba uzungumzavyo na Kerr hata sisi huwa tunazungumza naye kwa njia nyingine.


Mwandishi wa makala hii ndiye mmiliki wa BOIPLUS BLOGSPOT, anapatikana kwa namba;
0788334467
E-mail: boiplus.blogspot@boi.co.tz

Post a Comment

 
Top