BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
LEO ni siku ya maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika, kwa mwaka huu yamefanyika kwa namna tofauti kabisa na miaka mingine ambapo imezoeleka kuona sherehe kubwa na maonyesho ya silaha za kivita. Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli aliamuru siku hii kusiwe na shamrashamra zozote, badala yake iadhimishwe kwa wananchi kufanya usafi wa mazingira.Mshambuliaji wa Jomo Cosmos ya Afrika ya Kusini anayechezea Royal Eagles kwa mkopo, Uhuru Seleman, alizaliwa siku kama ya leo miaka 25 iliyopita. Na hii ndio sababu ya wazazi wake kumpa jina la Uhuru.

BOIPLUS ilimtafuta Uhuru na kufanyanae mazungunzo katika siku yake hii muhimu ya kuzaliwa.

MAMBO KIBAO ILA ANACHOJIVUNIA NI KUMUDU KULEA FAMILIA YAKE TU
Uhuru ambaye amemuoa Jamillah na kufanikiwa kupata watoto wawili, Nassir (4) na Nasriya (2) ana familia ya watu 13 ambao wanamtegemea yeye kwa kila kitu. Furaha yake kubwa ni kuona kipaji chake kimemfanya amudu kuwahudumia kwa kiwango stahiki.

"Kuna mambo kadhaa nimefanya kutokana na mpira, lakini katika umri huu ninachojivunia sana ni kumudu kuendesha maisha ya familia inayonitazama, namshukuru sana MUNGU kwa hilo". Alisema Uhuru.NYUMBA MBILI, USAFIRI, BIASHARA
Ishara za mafanikio mara nyingi huanzia kwenye upatikanaji wa huduma muhimu za kibinadamu ambazo ni Chakula, Mavazi na makazi (malazi). Uhuru tayari  ameshajikomboa kwa kujenga nyumba mbili ambapo moja ipo jijini Dar Es Salaam na nyingine Mbeya ingawa hakuwa tayari kutaja maeneo zilipo nyumba hizo.

"Nina nyumba mbili, hapo Dar na Mbeya, lakini pia namudu kufanya biashara ndogo ndogo za kujiongezea kipato". Aliongeza Uhuru.

SIKUDANGANYA UMRI, KWAHIYO BADO NINA MIAKA KIBAO YA KUCHEZA
Kuna tatizo kubwa miongoni mwa wacheza soka hasa barani Afrika, tatizo la kudanganya umri. Kwa upande wa Uhuru yeye anasema anafurahi kuona umri uliopo kwenye pasi yake ya kusafiria ndio umri wake sahihi, hajadanganya kama wengi wanavyofanya.

"Hapana sijadanganya umri, huu ni umri wangu halisi, kwahiyo bado nina miaka mingi sana ya kucheza soka. Nilianza kucheza soka la ushindani mwaka 2007 na hadi sasa bado najiona nina nguvu sana ya kucheza zaidi na zaidi". Alisisitiza Uhuru.ANAJIANDAA KUVUNJA MKATABA NA COSMOS ILI AENDE NJE YA AFRIKA
Katika umri wa miaka 25 Uhuru anaamini ni wakati muafaka wa kutoka nje ya mipaka ya Afrika na kwenda kujaribu bahati yake barani Ulaya au kwingineko. Uhuru aliiambia BOIPLUS kuwa yupo kwenye mipango ya kuvunja mkataba na Klabu yake ya Jomo Cosmos ili awe huru.

"Nataka nivunje mkataba na Cosmos ili niwe huru, hii itanisaidia kupata urahisi wa kutimka zangu nje ya Afrika". Alisema Uhuru ambaye anafanya vizuri na Royal Eagles huku akiwa amepania kuhakikisha anaipandisha timu hiyo hadi ligi kuu ya Afrika ya Kusini PSL.WACHEZAJI WA BONGO KUWENI MAKINI NA AFYA ZENU, ILA KIINGEREZA NACHO MUHIMU
Akijibu swali la mwandishi wa BOIPLUS juu ya ushauri wake kwa wachezaji hapa Tanzania, Uhuru alisema kama wanataka mafanikio basi wachezaji hao wanapaswa kujitambua, kujali afya zao huku akisema kuna changamoto kubwa wanakutanayo wakitoka nje, nayo ni lugha ya kiingereza.

"Wajitambue na kujituma, wajali afya zao kwa maana ni muhimu sana kwa mustakabali wa vipaji vyao, lakini pia wakipata nafasi wajifunze lugha ya kiingereza, ni changamoto kubwa sana kwetu huku ugenini.

BOIPLUS inamtakia Uhuru kila la heri katika siku yake hii muhimu.

Post a Comment

 
Top