BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
IMEDAIWA kuwa watu 60 wamefariki dunia juzi Ijumaa katika machafuko ya kisiasa nchini Burundi ambapo mke wa beki wa Simba, Emiry Nimubona amenusurika kwenye machafuko hayo ambayo yalifanyika kwenye mtaa anaoishi Nimubona na familia yake.

Jana kocha wa Simba, Dylan Kerr alimpanga Nimubona kwenye kikosi cha kwanza huku Hassan Kessy akianzia benchi lakini beki huyo amesema kuwa alicheza mechi hiyo akiwa na mawazo mengi juu ya familia yake ambayo inaishi kwenye mazingira magumu.


Nimubona alisema kuwa kwa kiwango alichocheza alijitahidi sana ingawa anafahamu kuwa mashabiki na wapenzi wa Simba walihitaji afanye mambo makubwa zaidi lakini alijikuta akili yake ikikwama kabisa hasa alipokumbuka yanayojiri nchini mwake.

"Mashabiki wameona kosa nililolifanya pekee ila hawajaona ushindi wa goli la kusawazisha niliochangia, nafahamu hawajui nini kinanisibu, walikuwa wanataka nipige krosi baadaye hawanisadii kukaba, ila kusema ukweli kichwa changu hakikuwa kwenye mechi hiyo.

"Hali ya Burundi ni mbaya, machafuko ya kisiasa yamefika mpaka mtaani kwetu ambapo watu 60 wameuwawa na mke wangu pamoja na familia wamenusurika ingawa waliingia mpaka kwangu, naamini kama ningekuwa nimepatiwa nyumba ningehamisha familia yangu ili akili iwaze jambo moja la mpira, sijui nyumba nitakayopewa kama nitaweza kuleta familia yangu," alisema Nimubona.

Machafuko hayo yanatokana baada ya rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunzinza kulazimisha kugombea awamu ya tatu kwenye uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Post a Comment

 
Top