BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo leo imempa baraka zote straika wa TP Mazembe na Taifa Stars, Mbwana Samatta kuelekea kwenye kinyang'anyiro cha tuzo ya Mchezaji Bora Afrika ambazo fainali zake zitafanyika Januari 5 mwakani.


Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake Waziri wa wizara hiyo, Nape Nnauye alisema kuwa Samatta amekuwa akiiwakilisha vyema Tanzania na ana kila sababu ya kutwaa tuzo hiyo ambayo Samatta ameingia kwenye tatu bora.

''Nampongeza sana Samatta kwa mafanikio aliyoyapata kupitia soka ni mafanikio yake lakini ni ya nchi nzima kwani anatuwakilisha vyema, naamini hata hii tuzo kubwa atatwaa pia hivyo watanzania wote tuungane kumwombea ili ashinde,'' alisema Nnauye na kuongeza.

''Kikubwa ambacho serikali ya sasa inakifanya ni kupambana na wajanjawanja walioingia kwenye sekta hii ya michezo ambao wanawanyonya wachezaji wanaotumia nguvu nyingi uwanjani, tunataka wanamichezo wanufaike pamoja na serikali,'' alisema


Naye Samatta alisema kuwa ''Nipo tayari kufanyakazi na serikali ili kuleta maendeleo ya soka nchini, kikubwa naomba baraka zenu ili nifanikiwe zaidi,''.

Samatta pia anatarajia kusaini mkataba wa miaka minne na nusu na timu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji kwa mkataba wenye thamani ya Euro 2.5 milioni.

''Kila kitu kinakwenda sawa ila nasubiri kusaini mkataba huo mara baada ya wao kumalizana na timu yangu ya TP Mazembe huo ndiyo utaratibu uliopo naamini itakuwa mapema tu mwezi ujao,''

Post a Comment

 
Top