BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Ally Shatry 'Chico', Shinyanga
SIMBA leo imepata pointi moja katika mechi yake ya pili ya Ligi Kuu Bara baada ya kutoka sare na Mwadui FC ya Shinyanga, mechi iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mkoani humo.

Hii ni mechi ya pili kwa Simba kulazimisha sare Kanda ya Ziwa ambapo mechi ya kwanza walitoka sare na Toto African ya Mwanza kwa bao 1-1.


Matokeo hayo ni mazuri kwao lakini si mazuri katika msimamo wa ligi kwani yanaifanya timu hiyo iendelee kushika nafasi ya nne kwenye msimamo huo wakiwa na pointi 24 huku Mtibwa Sugar wakibaki nafasi ya tatu wakiwa na pointi 27 baada ya kuifunga  Mgambo JKT bao 3-0, mechi iliyochezwa uwanja wa Manungu, Morogoro.

Mwadui ndiyo walikuwa wa kwanza kutikisa nyavu za Simba kupitia kwa kiungo wao Nizar Khalfan katika dakika ya 77 huku Simba ikipata bao la kusawazisha dakika ya 84 mfungaji akiwa ni winga Brian Majwega huku wakiwa wamepoteza nafasi nyingi ambazo zingewapatia mabao.

Mwadui ambayo ipo chini ya Kocha Jamhuri Kihwelu 'Julio' ambaye alitumia mfumo wa kujihami zaidi na Simba kushindwa kupenya ngome ya wapinzani wao waliokuwa nyumbani.


Dylan Kerr alifanya mabadiliko katika kikosi chake ambapo aliwatoa Said Ndemla na Hamisi Kiiza nafasi zao zilichukuliwa na Majwega pamoja na Raphael Kiongera.

Matokeo mengine katika mechi za leo Stand United imeifunga Coastal Union bao 3-1, mechi iliyochezwa uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Prisons imeilaza Majimaji bao 2-0.

Ndanda ambao walikuwa wenyeji wa JKT Ruvu wamekubali kichapo cha bao 3-1, mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Post a Comment

 
Top