BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
STRAIKA Amissi Tambwe raia wa Burundi leo amefanya yake kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kupiga hat-trick timu yake ya Yanga ilipoilaza Acacia Stand United bao 4-0.

Acacia Stand United ilikosa nafasi nyingi za wazi huku Yanga wao wakitumia vizuri nafasi walizozipata na kufanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao matatu pamoja na pointi tatu zilizowafanya waendelee kukaa kileleni wakiwa na pointi 30.


Tambwe alianza kucheka na nyavu za wapinzani wao dakika ya 18 baada ya Thaban Kamusoko kupiga mpira uliomkuta kipa wa Stand, Frank Muwange ambaye alirudisha mpira ndani na kumkuta Tambwe aliyetupia nyavuni.

Dakika ya 29, Elius Maguli aliikosesha timu yake bao baada ya kupiga shuti lililotoka nje kidogo ya goli ambapo Tambwe alicheka tena na nyavu dakika ya 36 bao alilofunga kwa kichwa.

Acacia Stand United, ilikosa bao lingine kupitia kwa kiungo wao Harun Chanongo ambaye pia alipiga shuti kali na kugonga mwamba akiwa yeye na kipa Deogratius Munishi 'Dida'.

Tambwe aliwainua tena mashabiki wa Yanga katika dakika ya 45 na kuifanya Yanga ambao ni Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao hayo matatu.

Dakika ya 66, Kamusoko aliipatia Yanga bao la nne ambalo alifunga kwa kichwa ukiwa ni mpira wa krosi na ndipo kocha wa Acacia Stand United, Patrick Leiwig aliamua kufanya mabadiliko ya kuwatoa Maguli, Amri Kiemba na Abuu Ubwa ambao nafasi zao zilichukuliwa na Frank Khamis, Jeremiah Katula pamoja na Seleman Mrisho

Kocha wa Yanga, Hans Pluijm aliamua kuwatoa Donald Ngoma na Kelvin Yondan nafasi zao zilichukuliwa na  Matheo Anthony na Pato Ngonyani

Mwamuzi wa mchezo huo Ludovic Charles alitoa kadi nyekundu kwa mchezaji wa Stand United, Katula katika dakika ya 90 baada ya kumfanyia madhambi Tambwei.

Post a Comment

 
Top