BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
UONGOZI wa Mwadui FC umesema kuwa kuondoka kwa straika wao Paul Nonga ni pigo lakini umewapa jukumu la kuziba pengo hilo Rashid Mandawa na Jerryson Tegete.

Wiki hii Nonga amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga akiwa amebakiza miezi sita kwenye klabu ya Mwadui ambapo Yanga walilazimika kuilipa Mwadui ili wamwachie mchezaji huyo ambaye ameifungia Mwadui mabao manne mpaka sasa.Katibu Mkuu wa Mwadui, Ramadhan Kilao, alisema kuwa Nonga ni mchezaji mzuri lakini wasingeweza kumzuia kuondoka kwani wanatambua maisha halisi ya wachezaji kwamba anapopata bahati kwa dau kubwa anatakiwa apewe nafasi.

"Tumelipwa fedha zetu na Yanga, ila tumemwambia Nonga kama ataona maisha ya huko ni magumu basi milango ya kurudi kwetu ipo wazi, tutakosa huduma yake lakini kuna wengine wataziba pengo lake naamini hatutayumba sana," alisema Kilao

Nonga ameondoka Mwadui akiiacha nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara huku ikiwa imekusanya pointi 18 na amejiunga na Yanga ambayo iko kwenye mbizo za kutetea ubingwa wake ikiwa imepanda kileleni kwa kufikisha pointi 27 wakati Azam wana pointi 26.

Post a Comment

 
Top