BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi 'Mido' na Ally Shatry 'Chico'
SIMBA leo imeshindwa kuonyesha makucha yake mbele y Toto African ya jijini Mwanza baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 22 kupitia kwa mshambuliaji wao Danny Lyanga huku Toto ikisawazisha dakika za nyongeza mfungaji akiwa ni Evarist Bernard ambaye aliingia kuchukuwa nafasi ya Miraji Athuman dakika ya 71.


Kocha wa Simba Dylan Kerr aliwatoa Ibrahim Ajibu, Hamisi Kiiza nafasi zao zilichukuliwa na Raphael Kiongera na Mwinyi Kazimoto.

Timu zote hazikuonyesha kiwango cha soka zuri kutokana na uwanja huo kujaa maji yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyeesha jijini Mwanza.

Matokeo mengine katika mechi za leo Prisons nao wamelazimisha sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar, mechi ambayo imechezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kuifanya Mtibwa ibaki nafasi ya tatu kwa pointi 24 huku Simba ikibaki nafasi ya nne kwa pointi 23.


Katika Uwanja wa Mwadui Complex, wenyeji Mwadui wameifunga Ndanda FC mabao 2-1, mabao ya Mwadui yalifungwa na Jerry Tegete na Jabir Azizi wakati bao la Ndanda lilifungwa na Atupelek Green huku Kagera Sugar ikiifunga African Sports bao 1-0, bao lililofungwa kwa penalti na Salum Kanoni.

Azam wao wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 26 na wamecheza mechi 10 ambapo kesho watacheza na Majimaji kwenye Uwanja wa Majimaji uliopo Songea.

Post a Comment

 
Top