BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
SIKU zote biashara ya silaha inakuwa chungu pale unaposhtuka uliyemuuzia ni adui yako vitani. Na hapo ndipo unapoweza kufunga kwa maombi ili silaha ulizomuuzia zisiwe kali. Zikiwa kali na zenye madhara basi kifuatacho ni kilio na kusaga meno.

Leo katika uwanja CCM Kirumba jijini Mwanza utapigwa mpambano wa Ligi Kuu ya Vodacom wakati wenyeji Toto Africans 'Wana Kishamapanda' watakapowakaribisha Wekundu wa Msimbazi, Simba.Mechi hii ina mvuto wa kipekee si tu kwa vile Toto iko na morali ya juu  baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 5-1 ugenini dhidi ya Majimaji ya Songea, au kwavile Simba iliambulia sare dhidi ya Azam jijini Dar es Salaam na kwamba sasa wamepanga kuanza kuweka pointi tatu kwenye akaunti yao kila baada mechi, mechi ina mvuto mwingine kabisa, nao ni kitendo cha mchezo huu kuwa ni kama mpambano wa mtengeneza silaha na mtumiaji.

Toto itaingia uwanjani ikijivunia nyota kadhaa ambao walipitia Simba na kung'aa katika michuano mbalimbali hasa ile ya BancABC Super 8. Katika michuano hiyo Simba ilipeleka kikosi chake cha pili ambacho kiliushangaza umma kwa kutwaa kombe hilo baada ya kuziadhirisha timu kadhaa kubwa zikiwemo Mtibwa Sugar na Azam.

Nyota kadhaa ambao waliipa Simba kombe hilo wamehamia jijini Mwanza wakiichezea Toto. Uwepo wa mabeki Waziri Hamad, Salum abdallah Chuku na  Hassan Khatibu, kiungo Abdallah Seseme na washambuliaji Miraji Athumani, Edward Christopher na Japhet Vedastus ambao wote walipitia Simba, unatosha kuubatiza jina mchezo huu na kuuita 'Simba Mtoto vs Simba Mkubwa'.Ni wazi kwamba vijana hawa wataongeza chachu ya mchezo huu si tu kwavile wanaijua Simba, lakini pia watataka kuuonyesha umma kuwa waliachwa kimakosa na kwamba bado wana uwezo mkubwa kuliko nyota waliopo Simba kwasasa.

Kwa miaka kadhaa Simba imekuwa ikipata wakati mgumu jijini Mwanza kwa kuishia kuambulia sare au kipigo kabla ya kubadilisha upepo msimu uliopita. Macho ya watanzania leo yatakuwa CCM Kirumba ambako utapigwa mchezo huo unaotarajiwa kujaa ufundi wa kila aina.


BOIPLUS ipo jijini Mwanza tayari kukuletea kila kitakachojiri kwenye mchezo huo.

Post a Comment

 
Top