BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
KOCHA wa timu ya Majimaji, Mika Lonnstrom raia wa Finland hatarudi kurudi kuifundisha timu kwa kile kilichodaiwa kuwa ni ukata unaoindama klabu hiyo huku baadhi ya wachezaji pia wakiingia mitini kwani hawajalipwa mishahara yao.


Chanzo cha habari kutoka ndani ya timu hiyo, kilisema kuwa ukata huo pia ulichangia timu yao kupoteza mechi dhidi ya Simba ambapo walifungwa bao 5-1 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kabla timu hizo hazijaenda kwenye mapumziko mafupi ya Ligi Kuu Bara ambapo jana pia walipokea kichapo cha bao 5-0 dhidi ya Toto African ya jijini Mwanza.

"Tuna hali mbaya kifedha na wengine wamegoma kujiunga na timu mpaka walipwe, tumecheza mechi yetu ya Toto ni kwasababu tulilazimika kucheza, hatukuwa na maandalizi yoyote na ndiyo maana tulifungwa, hakuna morali kabisa kwenye kikosi chetu," alisema mmoja wa wachezaji wa Majimaji

Kuhusu Kocha Lonnstrom yeye alisema kuwa "Bado nipo likizo na sijajulishwa kitu chochote na viongozi wangu kuhusu kurejea huko, hivyo siwezi kuzungumza zaidi kwasasa,"

Mwenyekiti wa Majimaji, Humphrey Milanzi alipoulizwa juu ya ukata unaoikabili timu yao alisema kuwa "Malipo ya kocha yapo tayari na tulimwekea pesa yake benki ila tuliambiwa tuhamishe kwenda kwenye akaunti yake ya benki huko kwao Finland, ila kocha atarejea muda si mrefu. 

"Wachezaji hawajaingiziwa mshahara wa mwezi uliopita pekee, bado tunahangaika kwa wadhamini kuhakikisha tunapata fedha ya kuwalipa wachezaji, hivyo watuvumilie mambo yatakaa sawa tu," alisema Milanzi.

Post a Comment

 
Top