BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
KLABU ya KRC Genk inayoshiriki ligi kuu ya nchini Ubelgiji ipo katika mazungumzo na TP Mazembe kuhusu kumnunua straika wake Mbwana Samatta aliyetwaa tuzo ya ufungaji bora Afrika mwaka huu.Taarifa ambazo BOIPLUS imezinyaka kutoka kwa mtu wa ndani ya Mazembe ni kwamba Rais wa klabu hiyo Moise Katumbi yupo nchini Ubelgiji kwa ajili ya mazungumzo na kama dili hiyo itakamilika basi Samatta atajiunga na wakali hao wa Ubelgiji mapema mwezi januari mwakani na kuwa ametimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kucheza Ulaya.

Mtandao  huu ulimtafuta Samatta ambaye yupo nchini kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka kutaka kujua zaidi kuhusiana na mpango huo. Samatta alikiri kuwa kuna mipango mingi inaendelea ila yeye hawezi kuambiwa hadi pale mmojawapo utakapokuwa tayari.

"Kwasasa sifahamu lolote kwavile viongozi wangu ndio wanashughulikia masuala ya uhamisho, kuna timu nyingi barani Ulaya zimeonyesha nia ya kunisajili. Kwahiyo kama hao Genk wameanza mazungumzo na viongozi ni jambo zuri, nadhani wakiafikiana basi watanijulisha"


Moise Katumbi kulia akizungumza na waandishi wa habari kutoka Tanzania


Samatta atamaliza mkataba wake ndani ya Mazembe mwezi januari mwakani na Katumbi aliiambia BOIPLUS ilipokuwa nchini DR Congo kuwa hatoongeza mkataba mwingine, badala yake anampa ruhusa ya kwenda kujaribu bahati yake barani Ulaya kwavile tayari ameifanyia Mazembe mambo mengi makubwa huku akisisitiza kuwa yeye mwenyewe ndiye atakayesimamia mchakato na kuhakikisha straika huyo anapata timu nzuri.

Post a Comment

 
Top