BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
BABU yangu aliwahi kuniambia "Ukitaka kumshinda adui yako, basi jifunze kwanza ubora wake kabla hujaangalia udhaifu wake". Nimeyakumbuka maneno yake wakati naanza kuandika Makala hii maalumu kwa ajili ya wachezaji wa Simba ambao ndio wapinzani wakubwa wa Yanga.

Kama hukufanikiwa kuutazama mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya African Sports na Yanga, uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijijni Tanga, basi tafuta hata kipande cha video ya mechi hiyo kinachoonyesha bao pekee la Yanga lililowekwa kimiani na kiungo Thaban Kamusoko katika dakika ya 94 ya mchezo huo, kwa maana ya ndani ya dakika tano za nyongeza.


Achilia mbali uzuri wa bao lenyewe lililofungwa katika mtindo wa 'baiskeli', habari kubwa hapa ni jinsi bao hilo lilivyotafutwa. Mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia timu mbalimbali barani Ulaya zikitoka nyuma kwa mabao kadhaa na kusawazisha na hata kupata ushindi ndani ya dakika chache tu  za mwisho za mchezo. Hii hutokana na jitihada na moyo wa kutokata tamaa wa wachezaji wa kulipwa barani Ulaya. Kwa Tanzania, Yanga ni mfano bora wa timu zinazopambana kwa dakika zote za mchezo bila kukata tamaa.

Nawafahamu Yanga kwa mchezo wao wa kutokata tamaa hadi filimbi ya mwisho, lakini katika mchezo wao dhidi ya African Sports niligundua jinsi wachezaji wao wanavyoshirikiana kwa lengo la kupata matokeo, walikuwa na uzalendo kwa timu na mashabiki. 

Katika dakika za mwisho, wachezaji wa African Sports, kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa timu za Tanzania, walianza kujiangusha na kuonyesha wazi wazi kuwa wanajaribu kupoteza muda ili mechi hiyo imalizike kwa sare ambayo kwao ingetosha kuwa matokeo bora. Wachezaji wa Yanga wakiongozwa na Kamusoko waliamua kusaidia kumbeba kwenye machela mchezaji mmoja wa African Sports na kumpeleka nje baada ya kuona  wahudumu wa Msalaba Mwekundu nao wakifanya kazi yao kwa kasi ndogo mno.

Hata baada ya dakika tisini kumalizika na mwamuzi wa akiba kuonyesha dakika tano za nyongeza, bado wachezaji wa Yanga hawakuonyesha kukata tamaa, waliendelea kulishambulia lango la Sports huku wakicheza kwa umakini mkubwa na kuonyesha kuna kitu wanahitaji kupata katika dakika yoyote ya mchezo huo.


Jitihada na umakini wao ulizaa matunda sekunde chache kabla mwamuzi hajapuliza kipenga cha mwisho. Mlinzi wa kushoto wa Yanga, Haji Mwinyi alikimbia na mpira upande wa kushoto kwa kujiamini na bila 'pressure' kutokana na muda kuwa umekwenda sana, akapiga krosi ambayo ilipanguliwa na kipa na kumkuta Donald Ngoma ambaye alizidi kuthibitisha kuwa wao ni wapambanaji kwa dakika zote na wapo kwa ajili ya matokeo ya timu. 

Ngoma alikuwa jirani sana na goli huku kipa akiwa amemsogelea, isingekuwa rahisi kwake kufunga kwa kichwa, angeweza kupaisha au kupiga mpira ambao ungedakwa kirahisi na kipa, alichokifanya ni kumpasia Kamusoko ambaye alikuwa kwenye nafasi nzuri zaidi na bila ajizi aliitumia nafasi hiyo kuipatia Yanga bao pekee lililowapa pointi tatu muhimu.


Simba ni mfano wa timu nyingi za Tanzania ambazo hucheza kwa papara kadiri dakika zinavyoyoyoma na hasa wakiwa aidha wako nyuma kwa idadi fulani ya mabao au wakiwa sare na wanatafuta ushindi. Mara nyingi hupoteza nafasi za wazi au mabeki kufanya makosa yanayosababisha  hatari langoni mwao. 

Kwa msimu huu Simba imepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Prisons huku ikitoka sare katika michezo miwili dhidi ya Azam na Yanga ambazo ziko juu yake kwenye msimamo wa ligi, haya si matokeo mabaya. Inaonyesha wazi Simba ina kikosi kizuri na bado ina nafasi ya kuchukua ubingwa. 


Lakini ukirudi kuitazama michezo hii mitatu ambayo haikupata matokeo mazuri, utaona wazi kuwa papara za wachezaji ziliwanyima ushindi, kukata tamaa kwa wachezaji kuliwafanya wapunguze kasi ya mashambulizi. 
Kitendo cha timu kukosa kabisa utulivu kiliwafanya Azam ambao hawakuwa vizuri wabahatike kupata sare. 

Hakika kuna mengi ya kujifunza kupitia uchezaji wa Yanga, hawa wamekuwa imara hata pale wanapokosa wachezaji wa viwango vya juu sana, juhudi za pamoja huwalinda, kupambana hadi dakika ya mwisho kuliwapa ubingwa msimu uliopita ambapo tulishuhudia mechi kadhaa wakiondoka na pointi tatu kwa mabao ya jioni kabisa.Katika tukio moja kwenye michuano ya Ligi kuu ya Hispania, La Liga msimu uliopita, wachezaji wawili wa Real Madrid walishtuka kila mmoja akirusha mpira wake uwanjani kwenye dakika za mwishoni za kipindi cha kwanza tu cha mchezo. Kilikuwa ni kichekesho lakini katika maana ya uzalendo na kuipigania timu, hilo lilikuwa ni jambo kubwa sana. 


Katika mchezo wa Simba dhidi ya Azam ilishuhudiwa mashabiki wa Simba wakimzomea mlinzi wao kisa kachelewa kurusha mpira katika dakika za majeruhi, hii ina maana gani?, kwamba mashabiki ndio wanakuwa hawajakata tamaa ila wachezaji wameshakata tamaa?

Wachezaji wa Simba, hata kama mliitazama mechi hii ya Yanga na African Sports, mnapaswa kurudia kuangalia video ya mechi hiyo, kuna somo zuri kwenu.

Post a Comment

 
Top