BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
JKT Ruvu imepanga kumpa adhabu straika wao, Saad Kipanga, kwa kile kilichoelezwa kuwa alikwenda kucheza mechi mchangani maarufu kama Ndondo wakati timu hiyo ikijandaa na mechi dhidi ya Coastal United jana Jumapili.


Imeelezwa kuwa Kipanga ambaye alisajiliwa akitokea Mbeya City, alitoroka kambini iliyokuwa imewekwa katika hoteli ya Ndege Beach na kwenda kuisaidia timu ya Vinyago yenye maskani yake Mwenge jijini.

Katibu Mkuu wa JKT Ruvu, Ramadhan Madoweka amesema kuwa Kamati ya Utendaji inatarajia kukutana kwa ajili ya kujadili suala hilo na kutoa uamuzi wa hatua gani za kinidhamu achukuliwe.

"Bado hatujamchukulia hatua yoyote ingawa ni kweli alikwenda kucheza mechi ya mchangani wakati tunajiandaa na mechi dhidi ya Coastal Union, kamati ya utendaji itakaa na kumuita mchezaji husika na kusikiliza utetezi wake kabla ya kuamua nini cha kufanya dhidi yake," alisema Madoweka.

Ikumbukwe kuwa kabla ya kutua JKT Ruvu, Kipanga aliwahi kusimamishwa na Mbeya City na kuamua kumpeleka Polisi Tabora ambayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza ili kupandisha kiwango chake.

Post a Comment

 
Top