BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
MSHAMBULIAJI wa Simba, Ibrahim Ajib jana aliumia katika mechi yao dhidi ya Mtibwa Sugar na kushindwa kuendelea na mechi hiyo lakini amewatoa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo ambao waliingiwa na hofu kwa kusema kuwa hawezi kukaa nje muda mrefu.

Ajibu alipata majeraha hayo baada ya kugongwa mbavu za nyuma ya mgongo na kiungo wa Mtibwa Sugar, Henry Joseph ambaye pia amesema kuwa hakukusudia kumchezea rafu mchezaji huyo kwani ilikuwa ni bahati mbaya katika purukushani za kuwania mpira.Ajibu alisema kesho anatarajia kwenda kufanya vipimo ili kujua ukubwa wa tatizo hilo na kama atatakiwa kupumzika ama kuendelea na mazoezi mepesi kwa siku kadhaa.

"Leo maumivu nayasikia kidogo tofauti na jana, ila kesho nitakwenda kufanya vipimo maana mpaka sasa sijui huko ndani kukoje, nikipata majibu ndiyo nitajua ukubwa wa tatizo na kama nitapumzishwa ama lah," alisema Ajibu

Kwa upande wa daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema: "Alipoumia tulijua kuwa inawezekana kaumizwa uti wa mgongo ila madaktari walimfanyia vipimo vya awali pale uwanjani na kugundua kuwa hakugongwa uti wa mgongo. Kwasasa anaendelea vizuri na huenda keshokutwa Jumanne akaanza mazoezi mepesi huku tukiendelea kumwangalia, mashabiki wasiwe na hofu,".

Post a Comment

 
Top