BOIPLUS SPORTS BLOG


KIKAO cha Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kilichoketi jana na kupitia taarifa mbalimbali za michezo ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) mzunguko wa pili, kimeiondoa timu ya Ashanti United kwenye michuano hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na Africa Lyon.

Katika kikao hicho kamati ilipokea malalamiko ya Africa Lyon dhidi ya Ashanti United kwa kumchezesha mchezaji Enock Balagashi kwa jina la Awesu Abdu katika mchezo namba 3, uliochezwa Disemba, 15 na Ashanti kuibuka na ushindi kwa mikwaju ya penati.

Kamati imejiridhisha baada ya kupitia taarifa ya mchezo huo, na kubaini klabu ya Ashanti United ilifanya udanganyifu wa kumtumia mchezji huyo kwa jina la mchezaji mwingine, huku ikitambua kuwa kufanya hivyo ni makosa na mchezo huo ulikuwa ukionyeshwa moja kwa moja kwenye kituo cha luninga cha Azamtv.

Kwa mujibu wa Kanuni no. 41 (12) ya uthibiti wa viongozi kufungiwa miezi 12, Kamati imemfungia Katibu Mkuu wa klabu ya Ashanti kutojihusisha na masuala ya mpira wa miguu kwa kipindi cha miezi 12.

Aidha Kamati pia kwa kutumia kanuni ya 37 (15) ya udhibiti wa wachezaji, mchezaji Enock Balagashi amefungiwa kwa kucheza mpira kwa kipindi ch amiezi 12 na faini ya Sh  300,000.

Kamati imezitaka klabu za ngazi zote nchini kuheshimu vipindi vya usajili kwa kufanya usajili wa wachezaji watakaowatumia, na kuheshimu kanuni na taratibu zinazoendesha michuano inayoandaliwa na TFF.

Africa Lyon watacheza dhidi ya Azam FC mzunguko wa tatu siku ya Jumatatu katika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

 
Top