BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu
AZAM FC imezifuata Simba na Yanga katika hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kuifunga African Lyon mabao 4-0 mechi iliyopigwa uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.


Tayari Simba na Yanga zilifuzu hatua hiyo baada ya kushinda mechi zao mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo Simba waliifunga Burkina Faso mabao 3-0 huku Yanga wakiifunga Friends Rangers mabao 3-0 pia.

Azam ilianza kuliona lango la Lyon dakika ya kwanza tu baada ya mchezo kuanza likifungwa na Mudathir Yahya huku Farid Musa akipachika bao la pili dakika ya tatu ambapo Farid aliongeza bao la tatu dakika ya 37 baada ya kupokea pasi nzuri ya Aboubakar Salum 'Sure Boy'.


Kipindi cha pili Kocha wa Azam, Stewert Hall alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Shomary Kapombe na John Bocco nafasi zao zilichukuliwa na  Khamis Mcha pamoja na Allan Wanga huku Lyon wao wakimtoa Omary Salum na Hood Mayanja nafasi zao  zilichukuliwa na Kassim Simbaulanga na Raizam.

Ame Ally aliiandikia Azam bao la nne dakika ya 54 akipokea pasi ya Farid huku Hall akimtoa nje Jean Mugiraneza 'Migi' na kumwingiza Said Morad wakati Lyon nao wakifanya mabadiliko yao kwa kumtoa John Simbeya nafasi yake ilichukuliwa na Abdallah Mguhi

Post a Comment

 
Top