BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally na Karim Boimanda
MCHEZAJI Bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza klabu za ndani, Mbwana Samatta leo amefunga safari mpaka jijini Lubumbashi ili amshawishi mmiliki wa TP Mazembe, Moise Katumbi  kumwachia akacheze KRC Genk ya Ubelgiji baada ya kuona mambo yanazidi kukwama.Wiki iliyopita ilielezwa kwamba serikali kupitia Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo imemalizana na Katumbi jambo ambalo limeelezwa kuwa si kweli kwani mmiliki huyo hajafanya mawasiliano yoyote na serikali ingawa imedaiwa pia kuna watu kesho nao watafunga safari mpaka Lubumbashi kumshawishi tajiri huyo alegeze uzi.

Katumbi amegoma kumwachia Samatta kwenda Genk na badala yake anataka ampeleke Nantes ambako bado straika huyo naye hajakubali kwenda na anapendelea zaidi kucheza Genk ambayo amesaini nayo mkataba wa miaka minne na nusu.

Samatta amekiri kwenda DR Congo kukutana na bosi wake na kwamba endapo bosi huyo ataendelea na msimamo wake huo basi itambidi aende Nantes kwani dirisha la usajili barani Ulaya linafungwa Januari 30.

Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo amethibitisha hilo na kwamba hayupo tayari kuelezea zaidi upande wa serikali ila wao wanapambana kumshawishi Katumbi akubali.

" Samatta ameondoka asubuhi ya leo kwenda Lubumbashi kwani huko ndiko kuna ajira yake, uwepo wake kule utasaidia kumshawishi Katumbi akubali kuwamwachia ili aende Genk akigoma basi tutajua cha kufanya hapo hapo baadaye vinginevyo yeye ndiye anaweza kuingia hasara.

"Bado kuna ugumu ndiyo maana Samatta amekwenda huko lakini kwa upande wa serikali hebu tuache jinsi ilivyo nao watafanya jitihada zao, hatutaki Samatta aende Nantes kwani kuna matatizo," alisema Kisongo.

Mkataba wa Samatta kuitumikia Mazembe unatarajia kumalizika Aprili na kama dili litashindikana itamlazimu kusubiri mpaka mkataba umalizike ili aondoke akiwa mchezaji huru.

Post a Comment

 
Top