BOIPLUS SPORTS BLOG

KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) iliyokutana Disemba 15 mwaka jana, imeiagiza klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia kuilipa Simba fedha za uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi ndani ya siku 60 kuanzia Januari 7, 2016.Katika taarifa hiyo ya FIFA na nakala yake kutumwa TFF, Etoile du Sahel na Simba, Kamati ya Nidhamu imefikia uamuzi huo baada ya klabu ya Etoile du Sahel kupuuza kuilipa klabu ya Simba kiasi cha dola 300,000 za uhamisho wa mshambuliaji Emmanuel Okwi uliofayika Januari 2014.

Katika barua hiyo ya maamuzi ya kikao hicho, Kamati ya Nidhamu imesema baada ya siku 60 zilizotolewa kwa klabu ya Etoile kuwa iwe imeilipa Simba kumalizika bila malipo hayo kuwa yamefanyika, wataagiza Etoile du Sahel kukatwa pointi sita katika michezo yake ya Ligi Kuu ya Tunisia.

Na kama klabu ya Etoile itashindwa kulipa deni hilo hata baada ya kukatwa pointi sita, Kamati ya Nidhamu ya FIFA itaamua kuishusha daraja klabu hiyo kutoka Ligi Kuu mpaka ligi daraja la kwanza.

Chama cha Soka nchini Tunisia (FTF) kimekumbushwa kutekeleza maelekezo hayo ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA ya kuipokonya pointi sita Etoile du Sahel, na endapo FTF itashindwa kufanya hivyo basi itafungiwa kujishugulisha na shughuli zote za mpira zinazosimamiwa na FIFA.

Kamati ya Nidhamu ya FIFA pia imeigiza klabu ya Etoile du Sahel kulipa faini ya dola 20,000 ndani ya siku 60 baada ya kupokea uamuzi huo wa kamati.

TFF imepewa jukumu la kuhakikisha Simba inalipwa deni hilo ndani ya muda uliopangwa wa 60 na endapo klabu ya Etoile du Sahel itashindwa kufanya hivyo basi TFF iitarifu kamati ya nidhamu ya FIFA juu ya suala hilo.

Kikao hicho cha Kamati ya Nidhamu kiliongozwa na Mwenyekiti Claudio Sulser (Uswisi), Makamu Mwenyekiti Kia Tong Lim (Singapore) na mjumbe Fiti Sunia (Visiwa vya Samoa)

Post a Comment

 
Top