BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu, Mtwara
BAO la dakika ya 81 la mshambuliaji Ibrahim Ajibu lilitosha kuipa Simba ushindi muhimu wa ugenini dhidi ya Ndanda FC kwenye mchezo uliomalizika jioni hii kwenye uwanja wa Nangwanda hapa Mtwara.

Ajibu alifunga bao hilo akimalizia vizuri mpira uliogonga mwamba kutokana na kichwa cha Hamis Kiiza aliyeunganisha krosi kutoka upande wa kulia iliyochongwa na Danny Lyanga.Shujaa Ajibu aliingia uwanjani mwanzoni mwa kipindi cha pili akichukua nafasi ya Rafael Kiongera ambaye ameanza kuitumikia Simba kwenye mzunguko wa pili baada ya kurudishwa kutoka KCB ya Kenya alikokuwa kwa mkopo.

Ndanda walianza vyema mchezo wa leo wakitawala mpira kwa asilimia kubwa ambapo walitumia vyema udhaifu wa Simba kwenye eneo la kiungo na dakika ya 8 tu, Atupele Green alifunga bao lililokataliwa akidaiwa kuwa ameotea akiunganisha krosi ya Omary Nyenje.

Pointi hizo tatu zinaweza kuokoa kibarua cha kocha Dylan Kerr ambaye inadaiwa kuwa alipewa mechi ya leo kuhakikisha timu hiyo inashinda baada ya kutoka sare kwenye mechi tatu mfululizo dhidi ya Azam, Toto Africans na Mwadui FC.Simba ilifanya mabadiliko kadhaa kwenye kikosi chake kilichocheza dhidi ya Mwadui mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kuwaanzisha Abdi Banda, Rafael Kiongera, Mwinyi Kazimoto na Emery Nibomana huku ikiwaweka nje ,Said Ndemla, Hassan Kessy na Ibrahim Ajibu.

VIKOSI

SIMBA; Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohammed Hussein, Abdi Banda, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Dan Lyanga, Mwinyi Kazimoto, Hamis Kiiza, Rafael Kiongera na Brian Majwega

NDANDA FC; Jackson Chove, Aziz Sibo, Kigi Makasi, Hemed Khoja, Ahmad Msumi, Salvatory Ntebe, Jackson Nkwera, Braison Rafael, William Lucian, Omary Mponda na Atupele Green

Post a Comment

 
Top