BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Nassoro Lufunga ametoa siku tatu kwa viongozi wa timu ya Stand United chini ya Mwenyekiti wao Amani Vincent uwe umefika ofisini kwake kukabidhiwa timu kama ilivyoamuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.

Hivi karibuni Nnauye alitoa agizo la kamati ya muda kurudisha timu mikononi mwa viongozi wa Stand United uliochini ya Amani.

Kabla hata ya Nnauye kuingilia kati mgogoro uliokuwepo ambao kiini chake kimeelezwa kuwa ni fedha hasa udhamini wa Kampuni ya Madini ya Acacia kuidhamini timu hiyo kwa Sh 2.4 bilioni kwa mkataba wa miaka miwili.


Leo Jumatano, mkuu wa mkoa huyo alifanya kikao kilichowakilishwa na baadhi ya watu kutoka Shirikisho la Soka nchini (TFF) ambapo Boniface Wambura alimuwakilisha Katibu Mkuu Celestine Mwesigwa aliyekwenda Nigeria kumpa sapoti Mbwana Samatta ambaye anawania tuzo ya Mchezaji Bora Afrika ambazo fainali yake ni kesho Alhamisi.

Wengine waliokuwepo ni watu wa ulinzi na usalama, wajumbe waliochaguliwa kutoka upande wa serikali kuunda kamati ya watu sita watakaosimamia matumizi ya fedha za udhamini huo ambapo kamati hiyo Mwenyekiti wake ni Amani.

Hata hivyo Amani na wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo hawakuwepo kwenye kikao hicho ambacho lengo kuu ni kuwakabidhi timu kwa mujibu wa agizo la waziri.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichoanza saa 8 mchana na kumalizika jioni zinasema kuwa baada ya viongozi hao kushindwa kuhudhulia kikao hicho, mkuu wa mkoa ametoa siku tatu wawe wamekwenda kukabidhiwa timu vinginevyo hatua nyingine itachukuliwa.

''Kwanza suala la udhamini hilo watajuwa wadhamini maana ndiyo waliopendekeza udhamini wao ushirikishe serikali, hivyo kwasasa timu ipo ipo tu mpaka watakapokwenda kukabidhiwa na kuiongoza wenyewe ingawa hakuna aliyewanyang'anya timu.

''Hatufahamu juu ya wadhamini kama watajitoa ama watabaki ingawa tulipewa onyo kuepuka migogoro ambayo utaweza kuwaathiri,'' alisema mmoja wa washiriki wa kikao hicho.

Kwa upande wa mratibu Mbasha Matutu ambaye anahusishwa na mgogoro huo alisema kuwa ''Mimi sio kiongozi wa klabu bali niliteuliwa kusimamia upande wa timu, hivyo mimi nafuata maelekezo yao na mkuu wa mkoa ametoa maelekezo hivyo yafuatwe hayo,''.


BOIPLUS inafahamu kuwa katika kikao hicho ilisomwa taarifa ya kocha mkuu, Patrick Leiwig, taarifa ya Mbasha pamoja na ya msemaji wa klabu, Deo Kaji Makomba.

Habari zaidi zinasema kuwa baada ya Stand United kucheza mechi yake ya mwisho dhidi ya Coastal Union, Leiwig aliwaambia wachezaji wake kuwa mgogoro unaondelea ndani ya klabu yao unaweza kuiathiri timu na kufika mbali kuwa hata mshahara wa mwezi huu huenda ukachelewa kuingia jambo ambalo liliwatia hofu wachezaji wake.

Hofu hiyo imepelekea wachezaji wa Stand kushindwa kujiunga na timu yao ambayo tayari imeingia kambini na mpaka sasa ni wachezaji 11 pekee ndiyo wamefika huku nyota wote wakisikilia hatima ya mgogoro huo.

Post a Comment

 
Top