BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Morogoro
KATIKA kile kilichoonekana kuwa Simba iko 'serious' na kombe la Shirikisho, leo imeifanyia kitu mbaya Burkina Faso ya Morogoro kwa kuitandika mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Jamhuri, Morogoro.Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu lakini hakuna timu ambayo ilifanikiwa kupata bao hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuliandama lango na Burkina ambapo katika dakika ya 58 nusura Emery Nimuboma aipatie bao la kuongoza baada ya mpira wake wa adhabu ndogo kugonga mwamba wa goli na kurudi uwanjani.

Ikionekana kama vile mchezo huo ungeisha kwa sare ya bila mabao, Hamis Kiiza 'Diego' aliwainua vitini mashabiki wa Simba baada ya kuipatia timu hiyo ya mtaa wa Msimbazi bao safi katika dakika ya 77 akimalizia vema krosi ya Danny Lyanga.Simba waliendelea kufanya mashambulizi kadhaa ambapo dakika za nyongeza, Said Ndemla alifumua shuti kali nje ya eneo la 18 na kufunga bao la pili. Dakika moja kabla mchezo haujamalizika Ndemla alifanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari hivyo mwamuzi Andrew Shamba akaamuru ilipigwe penati.
Kiiza alipiga penati hiyo na kuipatia Simba bao la tatu.

Katika mchezo, wachezaji wa Burkina  Hussein Shehe, Kessy Kessy, Jonathan Kishimba na Ulimboka Mwakingwe walipewa kadi za njano huku kwa upande wa Simba ni Hija Ugando na Hassan Kessy.

Simba iliwapumzisha Joseph Kimwaga, Mussa Mgosi na Emery Nimuboma huku nafasi zao zikichukuliwa na Ugando na Lyanga na Mwinyi Kazimoto. Burkina wao ilimpumzisha Kishimba na Hassan Mkota nafasi zao zikichukuliwa na Jumanne Wida pamoja na Athuman Jumanne.

Post a Comment

 
Top