BOIPLUS SPORTS BLOG

KOCHA mkuu wa Sønderjyske FC ya Denmark anayoichezea Mganda Emanuel Okwi, Jacob Michelsen, amesema mshambuliaji huyo amekuwa bora zaidi ya alivyokuwa akicheza Simba.


Akizungumza na mtandao wa Soka360, kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 17 (U17) alisema kuwa waliamua kumsajili Okwi baada ya yeye binafsi kugundua kipaji chake akiwa hapa nchini.

"Tulimsajili Okwi kwavile nilimuona hapo mara nyingi akiwa Simba, niligundua ni mchezaji mzuri na ambaye kipaji chake kinajionyesha wazi wazi, na ndio sababu tumempa mkataba mrefu," alisema

Michelsen ambaye ametangazwa kuwa kocha bora wa Denmark alimtabiria makubwa Okwi kuwa ni lazima atafanikiwa klabuni hapo na kwamba changamoto alizozipata mwanzoni ni za kawaida katika kuzoea mazingira. Na hiyo ni kutokana na tofauti kubwa iliyopo kati ya Ligi ya Denmark na Ligi kuu ya vodacom.

"Tunaamini atafanikiwa, miezi sita ya mwanzo ilikuwa ya kujifunza na kuzoea mazingira kwavile ametoka kwenye ligi ambayo ipo katika kiwango tofauti sana na ligi aliyopo sasa. Hii ina ufundi na nguvu zaidi ya alikotoka, kwahiyo bado hajaanza kwenye mechi za ligi hii.

"Amebadilika sana na sasa ni mchezaji bora zaidi ukilinganisha na wakati anawasili hapa, yuko fit zaidi na ana nguvu,'' alisema Michelsen

Katika dirisha dogo la usajili wa Ligi kuu ya Vodacom, Okwi alihusishwa na kurejea Simba lakini kwa taarifa hizi inaonyesha bado Sønderjyske ina mipango nae na kwamba anatengenezwa ili hata kama ni kuuzwa basi auzwe katika timu kubwa zaidi.

Post a Comment

 
Top