BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
KLABU ya TP Mazembe imemfungashia virago kocha wake Patrice Carterone raia wa Ufaransa aliyeiongoza Mazembe kutwaa ubingwa wa kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika mwishoni mwa mwaka jana kwa kuifunga USM Algers jumla ya mabao 4-1.


Mazembe wametoa taarifa hiyo ya kumtimua kocha wao kwenye tovuti yao ikieleza kuwa uamuzi wa Mazembe kumtema Carterone ulitolewa baada ya majadiliano ya kiungwana kati yake na mmiliki wa timu hiyo, Moise Katumbi na hiyo imetokana na timu hiyo kuboronga kwenye michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia.

"Baada ya kumalizika mashindano ya Klabu Bingwa Dunia nchini Japan, alitambua fika kuwa ameshindwa kukamilisha kazi yake kama ilivyoainishwa kwenye makubaliano ya kimkataba."

Mmiliki wa Mazembe, Katumbi inaonyesha alichoshwa na falsafa ya kocha huyo ya kuamini katika kupata matokeo mazuri badala ya kutafuta njia nzuri zitakazomwezesha kutimiza malengo yaliyowekwa.

Carterone ameifundisha Mazembe kwa kipindi cha miaka miwili kwa mafanikio makubwa huku ameondoka akiwa amewaachia taji la ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika pamoja na ligi.

Post a Comment

 
Top